Isa
From Wikipedia, the free encyclopedia
Isa ni umbo la jina Yesu katika Qurani na pia katika lugha mbalimbali zilizoathiriwa na Uislamu. Ukurasa huu unahusu imani ya Uislamu kumhusu Yesu kadiri ya Kurani.
Kitabu hicho kilichoandikwa miaka 600 hivi baada ya Kristo kina aya 93 zinazomhusu, lakini hakileti mfululizo wa habari za maisha yake wala za mafundisho yake maalumu.
Ingawa Waislamu wanakiri pia vitabu vitakatifu vya Torati, Zaburi na Injili, katika ibada wanatumia Kurani tu na kwa kawaida ndiyo chanzo chao cha habari juu ya watu na matukio ya kabla yake.
Kwao nabii Isa ni mtume anayeaminiwa kuwa mmojawapo wa mfululizo wa mitume na manabii watukufu 124,000 wa Mwenyezi Mungu walioletwa ulimwenguni kuwapasha wanadamu ujumbe wa umoja wake, ili wamuabudu Yeye peke yake akiwa ndiye Muumba na Mruzuku wao hapa duniani.
Mitume na Manabii hao wameletwa katika zama mbalimbali na kwa watu, kaumu na umma mbalimbali, na mfululizo huu ulianza na Adamu, baba wa wanadamu wote, hadi Mtume Muhammad akiwa ndiye wa mwisho.
Isa ni miongoni mwa mitume wakubwa ambao Mwenyezi Mungu amewasifu kwa subira yao na ustahimilivu wao mkubwa: Manabii Nuhu na Ibrahimu na Musa na Isa na Muhammad. Tena ni miongoni mwa Mitume waliopewa Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kiitwacho Injili. "Masihi Isa bin Mariamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Neno lake tu alilompelekea Mariamu, na ni Roho iliyotoka kwake" (sura ya 4 aya 171). Wakristo wanamuita kwa kawaida Yesu Kristo.