Moabu
From Wikipedia, the free encyclopedia
Moabu (kwa Kiebrania מוֹאָב Mo'av au Môʼāḇ, "Mbegu ya baba"; kwa Kigiriki Μωάβ Mōav; kwa Kiarabu مؤاب) ni jina la kihistoria la eneo la milimani upande wa mashariki wa Bahari ya Chumvi ndani ya nchi ya kisasa ya Yordani. Ilikuwako kati ya Edomu upande wa kusini na Amoni upande wa kaskazini.
Zamani eneo hilo lilikuwa ufalme wa Wamoabu. Mji wake mkuu uliitwa Diboni na maghofu yake yapo karibu na mji wa Dhiban wa kisasa.
Kati ya shuhuda za kiakiolojia za kabila hilo, muhimu zaidi ni Jiwe la Mesha, linaloeleza ushindi wao dhidi ya mwana wa mfalme Omri wa Israeli.
Sawa na Isreli Moabu ilikuja chini ya mamlaka kwanza ya Ashuru na baadaye ya milki ya Babeli. Mwaka 582 KK mfalme Nebukadnezzar II wa Babeli alifanya Moabu kuwa sehemu ya milki yake; hivyo ilikuwa sehemu ya ufalme wa Uajemi baadaye. Wakati wa utawala wa Kiajemi Moabu ilipotea kama taifa la pekee. Makabila ya Waarabu walianza kuingia na kukalia sehemu kubwa za nchi na wakazi waliacha lugha yao wakatumia Kiaramu badala ya lugha yao ya awali.