Mlima Kenya
From Wikipedia, the free encyclopedia
Mlima Kenya (Kikuyu: Kĩrĩnyaga; Kiembu: Kirenia; Kimaasai: Ol Donyo Keri; Kimeru: Kirimara) ndio mrefu zaidi nchini Kenya. Mlima huu una urefu wa mita 5,199. Mlima huu unatokana na volkeno zimwe ikikadiriwa ya kwamba mlipuko wake wa mwisho ulitokea mnamo miaka milioni 2.6 hadi 3.1 iliyopita.
Vilele vyake vya juu vinaitwa Batian (m 5,199), Nelion (m 5,188) na Lenana (m 4,985). Kuna barafuto nane mlimani lakini zinapungua kila mwaka kutokana na kupanda kwa halijoto duniani na kupungua kwa usimbishaji kwa sababu ya kukatwa kwa miti mingi[1][2][3].
Mlima Kenya ni volkeno rusu iliyoumbwa takriban miaka milioni 3 baada ya kuumbika wa Bonde la Ufa.[4] Umekuwa na theluji kwa maelfu ya miaka. Theluji hiyo hufanya kuwe na mmomonyoko unaosababishwa na barafuto na kutengeneza mabonde[5]. Barafuto zimepungua kutoka 18 hadi 10[3]. Mlima huu ni chanzo muhimu cha maji kwa Kenya.[6]
Habari kuhusu mlima zilifikishwa Ulaya mwaka 1849 na Ludwig Krapf,[7] lakini jamii ya wanasayansi walibaki na wasiwasi kuhusu ripoti kuwa kulikuwa na theluji karibu na ikweta.[8] Uwepo wa Mlima Kenya ulithibitishwa mwaka 1883 na 1887[9]. Ulipandwa na timu iliyoongozwa na Halford John Mackinder, mwaka 1899[10]. Leo Mlima Kenya hupandwa na watalii na wanaopenda kupanda milima na miamba.[11]
Mfumo wa ekolojia wa Mlima Kenya una aina tofauti za mimea na wanyama.[12] Mteremko hufunikwa na aina tofauti ya misitu. Spishi asilia ni kama vile mianzi, tai na pimbi.[13] Kwa sababu hii, eneo la km2 715 linalozunguka mlima ni Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kenya [14] na liliorodheshwa na UNESCO kama urithi wa dunia mwaka 1997.[15] Hifadhi (pori) hupokea wageni zaidi ya 15,000 kwa mwaka.[6]