Waiksosi
From Wikipedia, the free encyclopedia
Waiksosi (kwa Kiingereza Hyksos, kutoka Kimisri "heqa khaseshet", "watawala wa kigeni", kupitia Kigiriki Ὑκσώς, Ὑξώς, Yuksos) walikuwa watu mchanganyiko kutoka Asia Magharibi,[1] waliohamia mashariki mwa Delta la Nile kabla ya mwaka 1650 KK. Ujio wao ulikomesha nasaba ya kumi na tatu ya Misri na kuanzisha Kipindi cha kati cha pili.[2]
Uhamiaji wa watu kutoka Kanaani mwishoni mwa nasaba ya kumi na mbili ya Misri (1800 KK hivi) uliwatangulia Waiksosi wenyewe. Wakanaani hao waliunda ufalme wao huko wakati huohuo au mnamo 1720 KK.[3] Hiyo nasaba ya kumi na tatu ya Misri ilitawala mashariki mwa delta wakati mmoja na Nasaba ya kumi na tatu iliyotawala sehemu kubwa ya Misri.
Nguvu ya kutawala ya nasaba hizo ilififia taratibu, pengine kwa sababu ya njaa na tauni,[3][4]
Mnamo 1650 KK, nasaba zote mbili zilishindwa na Waiksosi, walioanzisha nasaba ya kuni na tano ya Misri, halafu wakaenea hadi kusini, walau kwa muda mfupi.[3]
Baadaye nasaba ya kumi na saba ya Misri iliteka Thebes na kutawala kusini, walau kama vibaraka wa Waiksosi.
Hatimaye Seqenenre Tao, Kamose na Ahmose I walipiga vita dhidi ya Waiksosi wakamfukuza kutoka Misri mfalme wao wa mwisho, Khamudi, mnamo 1550 KK.[3]
Waiksosi waliingiza Misri desturi zao mbalimbali, pamoja na teknolojia, muziki, mbegu za mimea na wanyama kutoka Asia.[5][5] Waliingiza vilevile farasi na magari kwa ajili ya vita.[6]