Biashara ya utumwa kupitia Atlantiki
From Wikipedia, the free encyclopedia
Biashara ya utumwa kupitia Atlantiki (vilevile: Biashara ya utumwa ya pembetatu au Biashara ya utumwa ya ng'ambo ya Atlantiki) ni jina la kutaja aina ya biashara ambayo ilikuwa ikifanyika baina ya mabara matatu, yaani, Afrika (upande wa magharibi), Amerika na Ulaya (hasa katika pande za magharibi mwa Ulaya).
Biashara ilihusisha hasa wafanyabiashara kutoka Ulaya ambao walikuja na bidhaa za viwandani na kuvibadilisha na watumwa na vitu vya thamani kubwa barani Afrika kama vile dhahabu, almasi, fedha na kadhalika ambapo wao walichukua watumwa na bidhaa nyingine na kwenda nazo Amerika.
Wakiwa huko, watumwa walizalisha malighafi za kilimo na madini ambapo Wazungu walizichukua na kuzipeleka Ulaya kwa ajili ya kutengenezea bidhaa nyingine.
Watumwa waliochukuliwa Afrika walisafirishwa kwa njia ya meli kupitia Bahari ya Atlantiki hadi huko Amerika ambapo walitiwa utumwani katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Mahusiano ya biashara ya namna hiyo yameunda "Umbo la Pembetatu" ambalo likaja kujulikana kama "Biashara ya Pembetatu".