Hati ya Milano
From Wikipedia, the free encyclopedia
Hati ya Milano, iliyopata jina kutokana na mji huo wa Italia ilipotangazwa mara ya kwanza, ilitolewa mnamo Februari 313 na makaisari Konstantino Mkuu (wa magharibi) na Licinius (wa mashariki).
Hati hiyo ilimaliza dhuluma za serikali dhidi ya Wakristo zilizodumu kwa karibu miaka 250, tangu Kaisari Nero alipozianzisha mjini Roma mwaka 64 BK.
Ustawi wa Kanisa uliendelea kiasi kwamba hao watawala Wapagani walilazimishwa kuwaachia raia wote uhuru wa dini.
Kwa sababu hiyohiyo, kabla ya hapo, mwaka 311 huko Nikomedia, Kaisari Galerius alikuwa ameshatoa hati ya kuwavumilia Wakristo.
Hati hii ilikwenda mbele zaidi, ikiondoa dharau na kuagiza Kanisa lirudishiwe bila gharama wala bughudha mali zake zote zilitaifishwa kwanza.
Hata hivyo, tofauti na wanavyodhani wengi, haikufanya Ukristo dini rasmi ya dola hilo kubwa, jambo ambalo lilitokea baadaye tu, kwa hati ya Thesalonike iliyotolewa na Kaisari Theodosi I tarehe 27 Februari 380.