Kiburi
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kiburi (kutoka neno la Kiarabu; kwa Kiingereza: hubris[1], hybris[2] na pengine excessive pride[3] pamoja na arrogance[4]) ni hamu isiyoratibiwa ya kujipatia ukuu dhidi ya wengine[5][6], pengine hata dhidi ya Mwenyezi Mungu[7]. Kiburi ni hisia na fikra zilizopotoka kuhusu ukweli na uhalisia wa mambo[8] .
Katika Biblia, shetani anatajwa kuwa na fikra za kuwa juu ya Mungu[9]; hakika huo ni upotofu wa hali ya juu sana, kwa kuwa haiwezekani kwa namna yoyote kuwa zaidi ya Mungu hata kwa mfumbo wa jicho moja, na matokeo yake ni ya kutisha[10][11]. Ni sawa na kusema mtoto amzae baba au mama yake. Haiwezekani chombo cha udongo kikawa na uwezo zaidi ya mfinyanzi kwa kuwa ni kizuri na kinavutia na kusifiwa na watu wengi, huku aliyekifinyanga hajulikani[12]. Kitabu cha Isaya 29:16 kinasema, "Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, 'Hakuna mfinyanga huyu'; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, 'Yeye hana ufahamu'?"
Katika Ukristo kiburi ndicho kilema kikuu cha roho ya shetani na binadamu aliyepotoka.