From Wikipedia, the free encyclopedia
Tamthilia (pia: Tamthiliya au Tamthilia-Mchezo, kutoka neno la Kiarabu تمثیل ) ni moja kati ya sehemu za utunzi wa hadithi au fasihi simulizi (ngano au hadithi) ambayo mara nyingi tunaona katika kumbi za maonyesho au kupitia televisheni, au tunasikia kupitia redio.
Tamthilia au mchezo mara nyingi huwa mazungumzo baina ya watu, na kwa kawaida huwa mchezo hatuutazami katika televisheni tu, bali hata kuna watu wengine hufuatilia kwa kupitia maandiko yenye tamthiliya hizo na kuzielewa vyema.
Watu tunaowaona wanafanya tamthilia ni waigizaji; katika ukumbi wa maonyesho husimama juu ya jukwaa na kuanza kutoa burudani yao huku watu wakiwaangalia (watazamaji) wanaweza wakawaona vyema kabisa.
Mwongozaji anawasaidia waigizaji kufanya kazi zao vyema, au anawaeleza namna ya mchezo jinsi unavyotakiwa kuchezwa.
Tamthilia ya leo hugawanyika katika sehemu/matendo ambayo yana vijisehemu (maonyesho). Kila onyesho huendeleza hoja kuu za tendo. Muungano wa matendo hujenga mtiririko wa maudhui na fani kwa kubainisha wahusika, mtindo na dhamira.
Tamthilia huhusisha mijadala na mazungumzo kati ya wahusika wawili na zaidi. Mazungumzo katika tamthilia huwa mafupi na yanajenga dhamira ya msanii mtunzi. Tofauti na mazungumzo ya kawaida, katika tamthilia huwa ya kasi na hufuata mkondo maalumu wa mawazo tofauti na yale ya kawaida ambayo hubadili mikondo.
Mijadala katika tamthilia hujenga migogoro ambayo ndiyo tegemeo la uigizaji. Wahusika wa tamthilia hujidhihirisha kwa maneno, mawazo na matendo yao na pia kwa jinsi mtunzi anavyowasawiri. Sifa zao hujionyesha jukwaani; kwa mfano: unene, utajiri, ufukara, ujasiri, woga n.k.
Tamthilia hutegemea sana ukamilifu wa mandhari jukwaani ili hadhira iiamini. Mapambo ya jukwaani sharti yalingane na dhamira ili yafanikishe uigizaji. Mapambo na mandhari: taa, giza, kicheko, kilio, kinaya, sauti mbalimbali hupatia tamthilia uhai kila inapoigizwa.
Jukwaa ndio uwanja wa kudhihirisha tamthilia nzima. Mpangilio wa jukwaa hufanikisha au kutatiza uigizaji. huweza kurahisisha/kutatiza uelewa wa tamthilia. Waigizaji wakinyimwa nafasi ya kuigiza kutokana na udogo wa jukwaa huenda uigizaji ukakwamishwa. Uteuzi, mpangilio na matumizi ya jukwaa ni sehemu muhimu katika uigizaji, ili kuwezesha ufanisi wa uigizaji, waandishi wa tamthilia hutoa mielekezo na maagizo.
Hadhira na waigizaji huletwa pamoja na uigiazaji. bila hadhira uigizaji haujakamilika, mwandishi huwa amelenga watu wanaokusanyika katika thieta ili wajionee maigizo. Hadhira huwa ni kiwakilishi cha jamii pana ambayo msanii hulenga hisia zao. Baadhi ya tamthilia hushirikisha hadhira kwenye dhana ya kando, kimatendo kama vile kuimba, kijibu maswali. Hadhira hujumuishwa kihisia kila mara. Bila hadhira, ari na hamasa ya uigizaji itakuwa haipo.
Brecht akichangia nadharia ya ukengeushi alisema kuna pengo kati ya hadhira na waigizaji. Kila kundi liko katika dunia yake; kwa mfano waigizaji hutenda mambo yao kama kwamba hakuna anayewaona au kuwasikia.
Tamthilia ya leo imebadilika kiwakati na kiutunzi ndiposa hadhira na wagizaji wakawa katika ulimwengu sawia na kushirikiana. Tamthilia huhusishwa na uigizaji. Tamthilia ya leo hujumuisha nyimbo, ngoma, hadithi, uzungumzi nafsia, kuchanganya ndimi n.k.
Nafasi ya uigizaji hutegemea wahusika. Licha ya kuwa viumbe wa msanii, wao huongozwa na fasiri za mwelekezi wa uigizaji na kufahamu kwao wanachoigiza na uigizaji wenyewe. Tamthilia moja inaweza kuigizwa tofautitofauti kwa kutegemea:
Ndiposa Pickening na Hoeper wakasema tamthilia ni kiuzi tu ilhali maigizo hubadilika na wakati.
Muundo wa tamthilia ya kisasa umeazima kutoka tamthilia za Kiingereza ambazo ziliathiriwa na tamthilia ya Ugiriki. Muundo huo huwa na sehemu tano:
Kuna aina nyingi za tamthilia, lakini kuna michezo ambayo inaonekana kuwa muhimu kupita yote:
Kwa kutumia muundo wa Shakespeare, waandishi waliandika tamthiliya kwa lugha ya Kiswahili na zilihusisha masuala ya Kiafrika. Wakati wa ukoloni, drama ilikuwa kwa ajili ya Wazungu na Waafrika wachache waliojua Kizungu. Baadaye, waandishi wazalendo waliotaka kuwasiliana na umma, iliwabidi watunge tamthiliya yao kwa lugha ya Kiswahili. Baadaye, licha ya tamthiliya kuzingatia matumizi ya lugha ya Kiswahili, walianza kuzitazama, kuchunguza na kuzifanyia majaribio.
Tamthiliya za awali, k.v. Wakati Ukuta na Heshima Yangu, hazikuwa na utohozi wa matumizi ya fani za sanaa za maonyesho ya jadi. Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1960, na mwanzoni mwa miaka ya 1970, tamthiliya zilianza kuonyesha mwelekeo mpya. Pia, falsafa na imani za Kiafrika kabla ya ubepari zilianza kudidimia kidogo.
Syango na Mazrui (1992) walipanga historia ya tamthiliya za Kiswahili katika vipindi vinne:
Baadhi ya tamthiliya hizo ni kama vile: Nakupenda Lakini... (Henry Kuria, 1957), Afadhali Mchawi, na pia Mgeni Karibu (Graham Hyslop, 1957), Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi (Ngugi 1961). Zilizungumzia masuala ya jamii chache zikiwa za upelelezi. Tamthiliya nyingine zilizungumzia masuala ya kutovunja sheria zikirejelea wakoloni. Pia zilibainisha mgongano baina ya jamii za makabila tofautitofauti. Nyingi zilikuwa na lengo za burudani. Pia ziliendelea kudunisha hadhi ya Waafrika ingawa ni za Kiswahili. Mwaka 1960 ndipo Little Theatres zilianzishwa kwa burudani ya Wazungu.
Tamthiliya hizi zilijaa maudhui ya kimapenzi, migogoro ya kitamaduni, maudhui ya kikoloni. Tamthiliya hizi ni kama vile: Wakati Ukuta na Kwenye Ukingo wa Thim (Hussein Ibrahim), Pambo (Peninah Muhando), na Tazama Mbele (Kitsau Jay).
Maudhui yalikuwa: masuala ya ukoloni, historia ya Waafrika katika mapinduzi, haki za wanyonge. Kwa mfano: Mzalendo Kimathi (Ngugi), Mkwawa wa Hehe.
Zilikuwa na mwamko mpya. Zilichunguza jamii za Afrika Mashariki kwa mkondo mpya. Zilizungumzia: ukoloni mamboleo, uongozi, siasa na matatizo mengine kama vile ufisadi, unyanyasaji, uporaji n.k. Kwa mfano; Aliyeonja Pepo (Faruk Topan), Mashetani (Ibrahim Hussein), Kilio cha Haki (Alamin Mazrui).
Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Tamthilia kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.