Ugonjwa wa uti wa mgongo
From Wikipedia, the free encyclopedia
Ugonjwa wa uti wa mgongo au Meninjitisi (kutoka Kiingereza "meningitis") ni uvimbe au inflamesheni ya tando zinazofunika na kuukinga ubongo na uti wa mgongo, sehemu inayojulikana kwa jumla kama meninjesi.[1]
Meningitis | |
---|---|
Mwainisho na taarifa za nje | |
Specialty | Neurology, infectious diseases |
ICD-10 | G00.āG03. |
ICD-9 | 320ā322 |
DiseasesDB | 22543 |
MedlinePlus | 000680 |
eMedicine | med/2613 emerg/309 emerg/390 |
MeSH | D008581 |
Meninjitisi inaweza kuwa ya hatari kwa uhai kwa jinsi inflamesheni hii ilivyokaribiana na ubongo na uti wa mgongo; kwa hiyo, hali hii imeorodheshwa kama dharura ya kimatibabu na inadai umwone daktari.[1][2]
Dalili kuu za ugonjwa huu zinazotokea mara nyingi ni maumivu ya kichwa na kukazika kwa shingo, pamoja na homa na kuchanganyikiwa kwa akili, kutapika na kutoweza kustahimili mwangaza (fotofobia) au kelele kali (fonofobia).
Mara nyingi watoto hudhihirisha dalili za pekee kama vile kizunguzungu na mwasho. Uwepo wa upele unaweza kuwa dalili ya kisababishi maalumu cha meninjitisi; kwa mfano, meninjitisi inayosababishwa na bakteria aina ya meningokokasi unaweza kuambatana na upele maalumu.[1][3]
Inflamisheni hii inaweza kusababishwa na maambukizi ya virusi, bakteria au vimelea wengine, na kwa kiasi kidogo na dawa fulani.[4]
Sindano ya mgongo husaidia kutambua uwepo au utovu wa meninjitisi. Sindano hii huingizwa katika mfereji wa uti wa mgongo ili kudondoa sampuli ya kiowevu cha mfumo mkuu wa neva (KMN), kinachofunika uti wa mgongo na ubongo. Sampuli hii huchunguzwa katika maabara ya kiuuguzi.[2]
Matibabu ya kwanza ya meninjitisi kali huhusisha antibiotiki zinazotolewa upesi, na wakati mwingine dawa za kukinza virusi. Kotisteroidi pia zinaweza kutumika kuzuia matatizo yanayofuatia inflamesheni iliyozidi.[2][3]
Meninjitisi inaweza kuchangia madhara makali ya muda mrefu kama vile uziwi, kifafa, hidrosifilasi na uwezo duni wa kiutambuzi, hasa isipotibiwa haraka.[1][3] Baadhi ya aina za meninjitisi (kama vile aina zinazohusishwa na meningokokasi, Haemophilus influenzae aina B, numokosi au maambukizi ya virusi vya machubwichubwi) zinaweza kuzuiliwa kwa chanjo.[1]