Utumwa barani Afrika
From Wikipedia, the free encyclopedia
Utumwa barani Afrika ulipatikana kwa muda mrefu. Sawa na maeneo mengine ya Dunia ya kale, mifumo ya utumwa na kazi isiyo huru ilikuwa kawaida katika sehemu nyingi za Afrika. Utumwa huo ulikuwepo kabla ya kufika kwa wanfayabiashara wa watumwa Waarabu na Wazungu.
Wakati Afrika ilipoingizwa zaidi katika biashara ya kimaifa ya watumwa, mifumo hiyo ya utumwa wa kimapokeo ilianza kupeleka wafúngwa pia kwa masoko ya watumwa nje ya Afrika [1]. Biashara hiyo ya kimataifa ilitokea katika biashara ya watumwa kuvukia Sahara, biashara ya watumwa katika Bahari Hindi, na biashara ya watumwa ya Atlantiki (ambayo ilianza karne ya 16).
Utumwa wa kimapokeo katika Afrika ulipatikana kwa aina tofauti: Utumwa wa deni, utumwa wa mateka wa vita, utumwa wa kijeshi, utumwa wa ukahaba, na utumwa wa jinai; vyote vilifanywa katika sehemu anuwai za Afrika. [2] Utumwa kwa madhumuni ya nyumbani na kwa mahitaji ya watawala ulienea kote Afrika. Utumwa wa mashambani ulitokea pia, hasa kwenye pwani la Afrika ya Mashariki na katika sehemu za Afrika ya Magharibi. Umuhimu wa utumwa wa mashambani ya ndani uliongezeka wakati wa karne ya 19, kwa sababu ya kukomeshwa kwa biashara ya watumwa ya Atlantiki na katika Bahari Hindi. [3] Madola kadhaa ya Kiafrika yaliyotegemea biashara ya watumwa ya kimataifa yalirekebisha uchumi wao kuelekea biashara halali ambako bidhaa zilizalishwa na watumwa. [4]