Kinjikitile Ngwale

From Wikipedia, the free encyclopedia

Remove ads
Remove ads

Kinjikitile Ngwale ni jina tata katika historia ya Tanzania. Mwanzoni mwa karne ya 20 aliwashawishi watu katika nchi inayojulikana sasa kama Tanzania kusimama na kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala nchi hiyo wakati wa ukoloni, akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza aliyodai kuwa na dawa ambayo ingewafanya wasiweze kudhurika.

Mtemi huyo wa kabila la Wangindo anachukuliwa kama ishara ya upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani huko Tanganyika. Kwa kuyaunganisha makabila ya eneo hilo na kadiri ujumbe wake ulivyozidi kusambaa, akachangia kuwa kati ya watu wa kwanza kuleta utaifa Tanganyika.[1]

Aliishi Ngarambe, eneo la Wamatumbi huko Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, sehemu ambayo kwa sasa ni kusini mwa Tanzania.

Akidai amepagawa na Hongo ambaye ni roho, aliwataka watu wa Tanganyika kuwapinga wakoloni kwa kuwaambia wafuasi wake kwamba iwapo watatumia maji yake yaliyo na dawa, risasi za Wajerumani hazingewaingia. Kulingana na mkongwe huyo, roho huyo alijitokeza kama nyoka, akamburuza Kinjiketile chini ya maji na alipoibuka baada ya saa ishirini na nne, alikuwa amekauka akaanza kutoa utabiri.[2][3][4]

Vita vya Maji Maji vilianza mwaka 1905 na kuisha 1907 na vilikuwa mojawapo ya vita vikuu dhidi ya ukoloni barani Afrika. Yeye anafahamika kama mwanzilishi wa vita hivyo, ingawa alikufa muda mfupi baada ya vuguvugu hilo kuanza, kwa kuwa alinyongwa mwezi Agosti mwaka 1905 na maafisa wa Ujerumani kwa kosa la uchochezi.[1][5]

Alikashfiwa kwa kuchangia vifo vya watu wengi baada ya kuwadanganya kwamba maji yangewakinga dhidi ya risasi. Inakadiriwa kwamba kati ya watu 180,000 na 300,000 walifariki dunia wakati wa vita vya Maji Maji kutokana na mapigano na njaa, jambo lililopunguza idadi ya watu kwa thuluthi moja.[6]

Mwaka wa 1969 mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Tanzania Ebrahim Hussein alichapisha mchezo wake "Kinjeketile" kuhusu maisha ya mwasisi huyo na vita vya Maji Maji.

Remove ads

Tanbihi

Loading content...

Marejeo

Loading content...
Loading related searches...

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Remove ads