Upatanisho wa imani na sayansi

From Wikipedia, the free encyclopedia

Upatanisho wa imani na sayansi ni juhudi zinazofanywa na watu wa dini mbalimbali kuondoa mzozo uliotokea kati ya imani na sayansi, hasa kuhusu suala la uumbaji kuhusiana na mageuko ya spishi. Juhudi hizo zinaitwa pengine kwa Kiingereza: theistic evolution, theistic evolutionism, evolutionary creationism, divine direction, au God-guided evolution[1].

Ieleweke mapema kwamba juhudi hizo hazilengi kutunga au kupitisha nadharia yoyote katika sayansi, ila kuonyesha uwezekano wa kukubali kweli zilizothibitishwa na utafiti wa sayansi pamoja na kweli zilizosadikiwa kwa kupokea ufunuo wa Mwenyezi Mungu.

Juhudi zinapingwa na wanasayansi wanaoshikilia uyakinifu na vilevile na watu wenye itikadi kali katika dini.

Asili ya suala hilo

Mzozo wa uumbaji-mageuko unahusisha mjadala unaoendelea na kuendeshwa hata katika utamaduni na siasa kuhusu asili ya Dunia, mwanadamu na wengineo. Zamani iliaminika bila shaka kuwa vyote vilivyopo viliumbwa vile vilivyo na vinavyoonekana. Katika enzi za sasa, na haswa baada ya mabadiliko ya karne ya 19, mageuko ya spishi kutokana na uteuzi maalumu unaotenda kazi kiasili katika viumbe au katika makundi ya viumbe yamethibitishwa na sayansi kuwa ndiyo msingi au chipuko na sababu ya dhati ya uhai na sifa zinazopatikana katika viumbe hivyo vya sasa au zilizopatikana katika viumbe enzi za kale. Kwa namna hiyo wapo wanasayansi wanaopinga imani na wapo wahubiri wa dini wanaopinga sayansi.

Kumbe watetezi wa upatanisho wa imani na sayansi wanaona si lazima uwepo upinzani kati ya hizo mbili kwa sababu kila moja inakabili masuala yake kwa namna yake. Yaani sayansi inachunguza ulimwengu na vyote vilivyomo kwa vipimo na utafiti wa kitaalamu, wakati imani inataka kupokea ufunuo wa Mungu ambao hauwezi kukanusha ukweli wowote[2][3][4].

Suala linavyojitokeza kwa kawaida

Mtu wa kwanza alitoka wapi ni swali ambalo wengi wanajiuliza bila kupata jibu la hakika. Kwa namna ya pekee wanafunzi wa shule wanapofundishwa katika historia kuwa mtu wa kwanza alitokana na kiumbehai mwenye asili moja na sokwe. Kumbe katika dini zao wanafundishwa kwamba mtu aliumbwa na Mungu. Hivyo wanajiuliza, lipi sahihi? Wapo wengi wanaodhani ni lazima kuchagua moja katika ya hayo mawili: ama kwamba mtu ametokana na kiumbehai aliyetangulia ama kwamba Mungu alimuumba mtu wa kwanza kama tulivyo sisi leo.

Katika sayansi

Sayansi imechunguza viumbehai waliopo duniani sasa na mabaki ya wale waliokuwepo zamani. Hasa baada ya kugundua DNA imeweza kuona uhusiano kati ya hao viumbehai mbalimbali. Hivyo imethibitisha kwamba mwili wa binadamu na ule wa sokwe imetokana na kiumbehai wa zamani (miaka milioni 5 au zaidi iliyopita) katika mlolongo wa mageuko ya spishi.

Lakini sayansi haiwezi kusema kitu juu ya roho, kwa sababu si mata, hivyo haipimiki. Zaidi sana haiwezi kusema lolote juu ya Mungu, kwa sababu si wa ulimwengu huu. Hata hivyo wapo wanasayansi wengi ambao walisadiki na wanasadiki dini fulani bila shida yoyote.

Katika imani na dini

Tofauti na itikadi kali katika dini, kuna mitazamo inayolenga kujumuisha au kupatanisha ujuzi kutoka maeneo haya mawili, yaani imani na sayansi. Ni kwamba wanaomuamini Mungu kama muumba wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana, si lazima wasadiki kwamba aliviumba vyote kama vilivyo sasa[5][6][7]. La sivyo wangeshindwa kueleza kwa nini watu wa leo wametofuatiana hivi kati yao, wakati wanaaminika wote kuwa watoto wa Adamu na Eva. Mabadiliko yaliweza kutokea kadiri ya maisha na mazingira yao, na bado yanazidi kutokea: kwa mfano leo watoto wanakuwa warefu zaidi.

Jambo la msingi kwa imani ni kwamba vyote asili yake ni Mungu tu aliyeviumba kwa hiari yake[8]. Hata leo Mungu anazidi kuumba watu na viumbe vingine, lakini anatumia wazazi wao, hawaumbi moja kwa moja. Ni vilevile kuhusu mtu wa kwanza: hata kama Mungu alitumia kiumbehai aliyetangulia katika kumuumba Adamu anabaki muumba wake kwa sababu hata kiumbe huyo alikuwa kazi yake kama ulimwengu wote ulivyo kadiri ya imani[9].[10]

Katika falsafa

Kuna wakati ni vigumu kulinganisha sayansi na dini. Dini inamhusu Mungu ambaye ndiye Mwanzo wa vitu vyote. Mwanafalsafa Emmanuel Kant alisema kinachoanza ni kitu kisichoonekana, na ndicho kinasababisha kitu cha wazi kutokea. Kama ni hivyo basi, sayansi na dini ni vitu viwili tofauti, ingawa vina uhusiano kama vile baba na mama ni watu wawili tofauti ingawa wanahusiana.

Tanbihi

Vyanzo

Marejeo mengine

Viungo vya nje

Loading related searches...

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.