Afrodita
mungu wa kike wa Kigiriki wa upendo, uzuri, raha, na uzazi From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Afrodita (kwa Kigiriki: Ἀφροδίτη, Afrodite) ni mmoja wa miungu kumi na wawili wa Olympia. Katika visasili vya Kigiriki, yeye ni mungu wa kike wa upendo, uzuri, na msisimko wa kingono, pamoja na uzazi wa kila aina. Aidha, anahusishwa na raha na nguvu ya kuamsha au kuua upendo katika mioyo ya wanadamu. Wasichana ambao hawajaolewa walimwomba awasaidie kupata waume, na pia aliaminika kuwapa watu uzuri wa kimwili na haiba ya kuvutia. Katika dini ya Roma ya Kale, analinganishwa na Venusi.
Kulingana na Hesiodo, Aphrodita aliumbwa wakati Kronos alipomhasi baba yake, Urano, kwa kutumia mundu na kukata viungo vyake vya uzazi, kisha kuvitupa baharini. Kutokana na kitendo hicho, povu lilianza kuibuka juu ya maji, na kutoka humo alitokea Aphrodita, akipelekwa na bahari hadi Kupro au Kithira. Hivyo basi, mara nyingine aliitwa Mkupro na wakati mwingine Mkithira. Hata hivyo, Homeri anadai kwamba alikuwa binti wa Zeu na Dione.
Katika visasili vya Kigiriki, Afrodita aliolewa na Hefesto, mungu wa moto, wahunzi, na usanii wa chuma. Hata hivyo, Afrodita mara nyingi hakuwa mwaminifu, kwani aliwahi kuwa na wapenzi wengi na kumdanganya mumewe mara kwa mara; katika Odisei, alikamatwa akifanya uzinzi na Aresi, mungu wa vita. Katika Wimbo wa Kihomeri kwa Afrodita, alimshawishi mchungaji wa kawaida aitwaye Ankisi, baada ya Zeu kumfanya ampende. Afrodita pia alikuwa mama mbadala na mpenzi wa mchungaji mwingine aitwaye Adoni, ambaye baadaye aliuawa na nguruwe mwitu.
Pamoja na Athena na Hera, Afrodita alikuwa mmoja wa miungu watatu wa kike ambao ugomvi wao ulisababisha mwanzo wa Vita vya Troia, na akaendelea kuchukua nafasi muhimu katika Iliadi. Afrodita ameonekana mara nyingi katika sanaa ya Magharibi kama alama ya uzuri wa kike na ameonekana katika kazi nyingi za fasihi ya Magharibi.
| Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Remove ads
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads