Bartolomeo Las Casas
From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Bartolomeo Las Casas, O.P., kwa Kihispania Bartolomé de las Casas (Sevilia, 1484 hivi – Madrid 18 Julai 1566) alikuwa mwanahistoria, mwanaharakati, mtawa wa Shirika la Wahubiri, askofu wa Kanisa Katoliki na mtu wa kwanza kutambulika rasmi kama "Mtetezi wa Waindio".

Maandishi yake mengi, yakiwemo Historia fupi ya uangamizaji wa Uindio na Historia ya Uindio, yanasimulia miongo ya kwanza ya ukoloni wa Hispania barani Amerika na kukazia hasa maovu ya wakoloni dhidi ya wenyeji.[1]
Remove ads
Maisha
Akiwa mmoja wa walowezi wa kwanza kutoka Ulaya, kwanza alishiriki, lakini baadaye alijisikia wajibu wa kupinga kabisa maovu hayo.
Mwaka 1515 alibadili mtazamo wake wa awali, aliachilia watumwa wake na haki zake, akatetea zile za Waindio mbele ya Kaisari Karolo V.
Katika maandishi yake ya kwanza alipendekeza Waafrika washike nafasi ya Waindio kama watumwa katika makoloni ya Amerika, na kwa sababu hiyo amelaumiwa kuchangia mwanzo wa Biashara ya ng'ambo ya Atlantiki.
Lakini baadaye alifuta pendekezo hilo, akitambua utumwa wowote ni mbaya sawia.
Mwaka 1522 alijaribu kuanzisha aina mpya ya ukoloni isiyo na ukatili kwenye pwani ya Venezuela, lakini aliposhindwa Las Casas aliamua kujiunga na utawa wa Wadominiko, akaacha shughuli za kijamii kwa miaka 10 hivi.
Baadaye alisafiri hadi Amerika ya Kati ili kuinjilisha kwa amani Wamaya wa Guatemala akashiriki mijadala kuhusu namna bora ya kuwaingiza Waindio katika Ukristo.
Aliporudi Hispania kutafuta wamisionari wapya, alizidi kupinga dhuluma hata akafaulu kufanya zipitishwe sheria mpya mwaka 1542.
Aliteuliwa kuwa askofu wa kwanza wa Chiapas, lakini baada ya muda mfupi ilimbidi arudi Hispania kutokana na upinzani wa wakoloni.
Miaka yake ya mwisho aliishi ikulu, akiathiri sera za Hispania kuhusu Waindio. Mwaka 1550 alishiriki mdahalo wa Valladolid dhidi ya Juan Ginés de Sepúlveda aliyedai Waindio si binadamu kamili, hivyo wanahitaji kutawaliwa na Wahispania wapate ustaarabu. Las Casas alipinga kabisa na kusema kuwatumikisha ni kinyume cha haki.
Bartolomeo Las Casas alitumia miaka 50 kupinga utumwa na dhuluma za ukoloni, akihimiza serikali kuwa na sera adilifu zaidi. Ingawa hakufaulu sana, walau alileta nafuu fulani na uzingatifu wa maadili. Kwa sababu hiyo Las Casas anahersabiwa mara nyingi kati ya watetezi wa kwanza wa haki za binadamu.
Remove ads
Tanbihi
Marejeo
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads