Mlima Nyiragongo
Volcano ya Kongo From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Remove ads
Mlima Nyiragongo ni volkeno yenye mwinuko wa mita 3,470 juu ya UB [1] iliyopo kwenye Milima ya Virunga iliyopo mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda. Mlima Nyiragongo ni sehemu ya Hifadhi ya Virunga ukiwa kilomita 12 upande wa kaskazini mwa miji ya Goma (Kongo) na Gisenyi (Rwanda).

Kwenye kilele cha mlima kuna kasoko yenye upana wa kilomita 2 iliyojaa ziwa la lava (zaha), yaani miamba ya moto yaliyo katika hali ya kiowevu.
Ziwa hilo la lava la Nyiragongo wakati mwingine limekuwa ziwa la lava kubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni. Kabla ya mlipuko wa mwaka 1977 lilikadiriwa na kina cha mita 600 kilichoshuka na kupanda tena.[2] [3] Mlima Nyiragongo na mlima jirani wa Nyamuragira ilikuwa chanzo cha karibu nusu ya milipuko yote ya volkeno katika historia inayojulikana barani Afrika. [4]
Remove ads
Historia ya milipuko
Hakuna habari zilizorekodiwa zamani, lakini tangu mwaka 1882, imelipuka angalau mara 34.
Kuwepo kwa ziwa la lava kulithibitishwa kisayansi mwaka 1948. [5] Wakati huo, lilikuwa na eneo la m² 120,000. Utafiti uliofuata ulionyesha kuwa ziwa lilibadilika na wakati kwa ukubwa, kina, na jotoridi.
Mlipuko wa 1977
Mnamo 10 Januari 1977 kuta za kasoko zilipasuka, na lava lilitoka nje na kutelemka katika muda wa saa moja. [6] Lava ilitiririka chini kwenye mtelemko wa mlima kwa kasi ya hadi kilomita 60 kwa saa.[7] Vijiji kadhaa viliungua moto na watu wasiopungua 600 waliuawa. [8]
Hali ya vijiji vingi kuwa karibu na mlima Nyiragongo huongeza uwezo wake wa kusababisha maafa asilia.
Milipuko ya 2002
Maziwa ya lava yalirudi kutokea ndani ya kasoko ya Nyamirongo kutokana na milipuko midogo mnamo 1982-1983 na 1994.
Mlipuko mwingine mkubwa wa volkeno ulianza mnamo 17 Januari 2002. Ufa wenye urefu wa kilomita 13 ulifunguka upande wa kusini wa mlima kuanzia kwenye kimo cha mita 2,800 ukashuka hadi majengo ya kwanza ya mji wa Goma kwenye kimo cha mita 1,550. Lava ilitiririka kutoka mashimo upande wa chini wa ufa ikatiririka kama mto wa lava wenye upana wa mita 200 hadi 1,000 na unene wa mita 2 katika mji wenyewe ilipopoa na kuganda.
Watu 400,000 walihamishwa kutoka mji kuvuka mpaka wa Rwanda wakikimbia Gisenyi, mji jirani upande wa Rwanda wakati wa mlipuko huo. Lava ilifika Ziwa Kivu[9] ambako ilisababisha hofu ya kutoka gesi sumu zinazolala kwenye vilindi vya ziwa jinsi ilivyowahi kutokea kwenye janga la nchini Kamerun mnamo 1986. Hii haikutokea, lakini wataalamu wa volkano wanaendelea kufuatilia eneo hilo kwa karibu. [10] Lakini hali iliyohofiwa haikitokea.
Karibu 245 watu walikufa katika mlipuko huo kutokana na kukosa hewa kwa uenezi wa dioksidi kabonia na majengo kuporomoka kwa sababu ya lava na matetemeko ya ardhi. [11] Lava ilifunika asilimia 13 ya eneo la Goma, karibu km² 4.7[12] na karibu watu 20,000 walibaki bila makao[13].

Mlipuko wa 2021
Mnamo 22 Mei 2021 iliripotiwa kuwa volkano hiyo imeanza kulipuka tena. [14] Lava ilikaribia uwanja wa ndege wa Goma.[15] Barabara kuu ya kuelekea Beni ilizuiliwa na lava. Wakazi wengi kutoka Goma walikimbia kuelekea mpaka wa Rwanda. [16] [17] Mlipuko huo ulisababisha vifo vya watu wasiopungua 15, vingi vyake vikisababishwa na ajali za gari katika uokoaji uliofuata. [18]
Remove ads
Marejeo
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads