Muujiza
From Wikipedia, the free encyclopedia
Muujiza ni tukio lisiloelezeka kisayansi kufuatana na sheria za maumbile.[1]

Matukio hayo yanaweza kufikiriwa yamesababishwa ama na Mungu au miungu, hata kupitia mtu wa dini, ama na nguvu nyingine zinazohusiana na ushirikina.
Hayo ni tofauti kabisa na matukio ambayo yanapatikana kwa nadra lakini yanaweza kuelezwa kisayansi ambayo watu wengine wakiyashangaa na kuyafurahia wanayaita miujiza.
Katika Ukristo
Wanateolojia Wakristo wanasema Mungu kwa kawaida anaacha sheria za maumbile zifuate mkondo wake, lakini anabaki huru kuziingilia anavyotaka kwa mipango yake.[2]
Injili zinasimulia baadhi ya miujiza ya Yesu. Ilikuwa mingi sana; hata hivyo Injili ya Yohane (21:25) inashuhudia kwamba michache tu imeandikwa.[3][4]
Kati ya miujiza hiyo, kuna mazinguo ya kufukuza pepo wachafu, uponyaji wa maradhi mbalimbali (homa, ukoma, safura, kupooza mkono au mwili mzima, kupinda kwa mgongo, kutokwa damu mfululizo, upofu, uziwi, ububu na vilema vingine), ufufuo wa wafu, na ushindi juu ya uasilia (kama kugeuza maji kuwa divai, kutembea juu ya maji ya ziwa, kutuliza dhoruba na kuzidisha mkate na kitoweo cha samaki).[5][6]
Kwa mamlaka yake aliyoliachia Kanisa, wafuasi wengi wa Yesu wamejulikana kama watendamiujiza, ingawa wao walimrudishia Mwenyezi Mungu sifa hiyo, wakijiona vyombo vyake tu.
Kanisa Katoliki kabla ya kumtangaza muumini mwadilifu sana aliyefariki dunia kuwa mwenye heri linadai uthibitisho wa muujiza mmoja, na kabla ya kumtangaza mtakatifu muujiza mwingine.
Tanbihi
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.