Kupanda kwa halijoto duniani
kupanda kwa sasa kwa wastani wa halijoto ya Dunia na kuhusiana na mabadiliko makubwa ya mifumo ya hali ya hewa From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Kupanda kwa halijoto duniani (ing. global warming) ni mchakato wa mabadiliko ya tabianchi yaliyotambuliwa na wataalamu tangu miaka kadhaa.

Mchakato huo ulianza pamoja na usambazaji wa viwanda duniani. Unaonekana kwa kulinganisha vipimo vya halijoto vinavyopatikana tangu miaka 150. Kupanda huku kunaleta mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoanza tayari kuathiri maisha ya watu na uhai kwa ujumla.
Kuna hofu ya kwamba mabadiliko hayo yataleta hatari kubwa kwa jamii.
Kati ya wanasayansi kulikuwa na majadiliano kama sababu za mabadiliko hayo ni shughuli za binadamu tu au kama kuna sababu asilia. Siku hizi wataalamu karibu wote hukubaliana ya kwamba sababu kuu ni kuchoma kwa makaa na mafuta katika viwanda, magari na vituo vya umeme kunakopuliza hewani gesijoto kama dioksidi kabonia.
Remove ads
Vipimo na data
Duniani kuna upimaji wa kisayansi wa halijoto tangu mwaka 1860. Kabla ya hapo kuna kumbukumbu ya hali ya hewa katika karne zilizopita kutoka mahali mbalimbali ambazo hazikusanifishwa wakati ule.
Leo hii wanasayansi wanatumia vipimo na taarifa za kale wakipiga makadirio juu ya hali ya hewa katika historia.
Hapo wanatumia pia mbinu kama kulinganisha miviringo kwenye mashina ya miti inayoonyesha miaka yenye mvua nyingi au kidogo au wanapima kiwango cha dioksidi kabonia kwenye barafu ya chini nchani yenye umri wa miaka 10,000 na zaidi.
Makadirio ya hali ya hewa hutofautiana, lakini kwa jumla kuna picha juu ya miaka 1,000 iliyopita. Watalaamu wanakubaliana ya kwamba mnamo mwaka 1000 kulikuwa na kipindi cha joto kiasi, tena kipindi cha baridi kiasi kuanzia mnamo mwaka 1600.
Lakini hakuna hakika bado juu ya athira duniani kwa sababu sehemu kubwa ya data ni kutoka upande wa kaskazini ya dunia.
Vipimo vya kisayansi vinavyopatikana vinaonyesha ya kwamba halijoto ya wastani duniani imepanda sentigredi 0.7 kati ya 1906 na 2005. Hii si kiwango kidogo; wakati wa zama za barafu kubwa miaka 100,000 iliyopita halijoto ilikuwa tu 6 °C chini ya wastani ya leo na hii ilitosha kufunika sehemu kubwa za Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini kwa mabapa manene ya barafu.
Dalili zote zinadokeza ya kwamba kupanda kwa halijoto kuliharakishwa tangu mwaka 1970 na kunaelekea kupanda zaidi.
Remove ads
Sababu za kuongezeka kwa halijoto
Katika majadiliano kuhusu asili ya kupanda kwa halijoto wataalamu walijadiliana sababu mbalimbali zilizotajwa. Kuna idadi ya sababu za kiasili ambazo zilizowahi kuathiri tabianchi ya Dunia katika kistoria ya miaka mamilioni kama vile mabadiliko katika kiwango cha mnururisho wa Jua unaofika duniani au milipuko ya volkeno. Lakini ilionekana sababu hizi zote hazikuweza kuathiri tabianchi kiasi cha kueleza mabadiliko yanayopimwa.
Siku hizi karibu wataalamu wote hukubaliana kwamba sababu ni kuongezeka kwa gesi kama dioksidi kabonia hewani kutokana na shughuli za binadamu hasa kuchoma makaa na mafuta ya petroli tangu mwanzo wa mapinduzi ya viwandani katika karne ya 19.[1]
Remove ads
Matokeo yanayotazamiwa
Wataalamu wanaonya ya kwamba kupanda kwa halijoto kunaweza kuleta mabadiliko kama yafuatayo:
- kuongezeka kwa halijoto ya angahewa kutaongeza pia halijoto ya bahari na kusababisha uvukizaji mkubwa utakaoleta mawingu na mvua za nyongeza duniani
- mikondo ya bahari itabadilika na kubadilisha hali ya hewa katika nchi nyingi
- sehemu kadhaa zenye jangwa zitapokea mvua lakini maeneo mengine yatakosa mvua, hivyo kuleta matatizo kwa kilimo na njaa kwa watu
- barafu kwenye ncha za dunia itaendelea kuyeyuka. Hii itasababisha kupanda kwa uwiano wa bahari, kuleta mafuriko kwenye pwani za dunia na kuhatarisha makazi ya watu karibu na bahari, hasa miji ya bandari na nchi za visiwani: nchi kadhaa kama Maldivi zitazama baharini na kupotea kabisa
- kwa jumla upepo na tufani zitaongezeka na kuwa kali zaidi
- magonjwa kama malaria yataongezeka kwa sababu mbu wanaopitisha ugonjwa watapata nafasi mpya katika sehemu zilizokuwa baridi mno kwao
Juhudi za kimataifa
Kutokana na hatari zinazotazamiwa na karibu wataalamu wote wa elimu ya tabianchi duniani Umoja wa Mataifa ulifanya jitihada za kuanzisha hatua za kisiasa za kupambana na hatari hizi. Tokeo lake ni Kongamano la Mfumo wa UM kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (en:United Nations Framework Convention on Climate Change) ya mwaka 1993 ambayo nchi 194 zilijiunga nayo.
Nchi wanachama ziliendelea kupatana hatua mbalimbali katika Itifaki ya Kyoto na Mapatano ya Paris kuhusu Tabianchi ya mwaka 2015 ambayo nchi wanachama ziliahidi kuchukua hatua maalumu ya kupakana kupanda kwa halijoto kwa kiwango chini ya angalau 2°C kwa wastani au hata 1.5°C ikiwezekana.
Remove ads
Tazama pia
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads