Ruge Mutahaba
Msimamizi wa talanta na mkurugenzi wa vipindi From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Ruge Mutahaba (Brooklyn, New York, Marekani, 1 Mei 1970 - Afrika Kusini, 26 Februari 2019) alikuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Vipindi wa Clouds Media Group [1] nchini Tanzania.[2][3] Pia alikuwa mwanzilishi wa nyumba maarufu ya kukuza vipaji vya sanaa iitwayo Tanzania House of Talents (THT)[4] iliyolea na kukuza vipaji vingi vya muziki kama Diamond Platnumz, Barnaba Classic, Mwasiti, Linah, Ditto, Ray C na kadhalika.
Ruge alikuwa mtu mwenye msukumo wa kuisaidia jamii kuupokea ujumbe wa maendeleo. Kati ya miradi yake mikubwa iliyoacha alama kuwa kwa vijana Tanzania ni Mradi wa Fursa alioufanya kwa kushirikiana na Clouds Media Group na wadau wengine wa maendelea kama UN Tanzania[5], Brela[6], SIDO[7], Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu[8], Wizara ya Afya kupitia mradi wake wa Nyumba ni choo na mashirika mengine binafsi.
Katika kupambana na ukosefu wa ajira[9] kwa vijana waliohitimu elimu ya juu, Ruge alianzisha darasa maalumu aliloliita School of Excellence and Innovation akishirikiana na msanii maarufu Nikki wa Pili na Hassan Ngoma[10] ambao wote ni wakuu wa wilaya kwa sasa. Darasa hilo lilijikita kufundisha ujuzi laini wa lazima kwa wahitimu wa elimu ya juu ambao haukufundishwa darasani lakini ni wa lazima kuwasaidia kupata ajira au kuanzisha biashara zao binafsi ifikapo mwaka 2020[11] kama ulivyopendekezwa na taasisi ya kimataifa World Economic Forum[12]. Ujuzi huo ulihusisha Utatuzi wa Changamoto Tata (Complex Problem Solving), Ushirikiano na Wengine (Coordinating with Others), Kufikiri kwa Kina (Critical Thinking), Usimamizi wa Watu (People Management), Majadiliano (Negotiation), Ubunifu (Creativity), Usimamizi wa Viwango (Quality Control) n.k.
Ruge alipenda kushiriki ujuzi wake na watu wengine, na kabla ya kufikwa na mauti alianza kuandika kitabu alichokiita "Jibu Rahisi sio Jibu Jepesi" alichokiandika akishirikiana na mwanafunzi wake Elias Tryphone [13].
Remove ads
Elimu
Ruge ni mtoto wa kwanza wa profesa Gelase Mutahaba na Christina Mutahaba; alipata elimu yake ya shule ya msingi mkoani Arusha darasa la kwanza hadi la sita, kisha akahamia Shule ya Msingi Mlimani ambako alihitimu elimu yake ya msingi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani mkoani Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha nne, na kidato cha sita katika shule ya sekondari Pugu. Alihitimu shahada ya Masoko kisha Shahada ya Sanaa katika Uchumi Chuo Kikuu cha San Jose huko Kalifornia, Marekani[14]
Remove ads
Taaluma
Aliporejea Tanzania kutoka Kalifornia ambako alihitimu masomo yake, Ruge alianza kutambulika kwenye jamii baada ya kuanza kufanya kazi na rafiki yake Joseph Kusaga ambaye alikuwa akiendesha Klabu yake ya usiku almaarufu kama disko iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Clouds Disco. Ushirikiano wao ulipelekea kuanzishwa kwa Clouds Media Group mjini Arusha ambayo, licha ya kuwa chombo cha habari na burudani kwa jamii, hasa vijana, ilifanya kazi ya kuhamasisha vijana wadogo wa Kitanzania kujiingiza katika kutafuta fursa na ujasiriamali ili kujiinua na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla wake.[14] Tokea maisha ya utotoni Ruge alikuwa mpenada muziki, lakini kipaji chake hakikuwa kwenye muziki peke yake. Alikuwa mchezaji mpira wa miguu (soka), alipewa majina mengi kwa kipaji hicho akicheza timu za mtaani, za Chuo Kikuu kuanzia Adanco na Summer Rangers na alifikia hatua ya kuchaguliwa katika timu ya mkoa wa Dar es salaam ya UMISETA. Pia alikuwa na kipaji cha kuandika. Vipaji vingine vyote havikuweza kunawiri kwani alikuwa na mapenzi na muziki zaidi.
Remove ads
Familia
Ruge Mutahaba hakuwahi kufunga ndoa rasmi lakini alikuwa na mahusiano na Zamaradi Mketema na walipata watoto wawili.[14] Pia alizaa wengine watatu na kufanya jumla ya watoto watano [15]
Maradhi na kifo
Ruge Mutahaba alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na tatizo la figo akapelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, ambayo pia rais wa Jamhuri ya Tanzania John Magufuli alimchangia shilingi milioni hamsini [16], hadi mauti yalipomfika tarehe 26 Februari 2019.[3][17][18]
Watanzania wengi waliopokea habari za kifo chake, akiwemo Rais John Pombe Joseph Magufuli[17], walishtushwa na habari za mauti yake na kutuma jumbe za kuguswa kutokana na mchango mkubwa wa Ruge katika tasnia ya habari na burudani, ubunifu katika mipango mikakati, kuendeleza vipaji vya vijana wa Tanzania, kuhamasisha ari ya ufanyaji kazi kwa bidii katika jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.[3]
Remove ads
Marejeo
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads