Haiti

From Wikipedia, the free encyclopedia

Haiti
Remove ads

Haiti, rasmi kama Jamhuri ya Haiti, ni nchi iliyoko katika Karibi, inayochukua theluthi ya magharibi ya kisiwa cha Hispaniola. Inapakana na Bahari ya Karibi na Bahari ya Atlantiki, na inapakana na Jamhuri ya Dominika. Ina idadi ya watu takriban milioni 11.7, ikiwa ya 81 duniani. Mji mkuu na jiji kubwa zaidi ni Port-au-Prince. Haiti imegawanyika katika mikoa 10 ya kiutawala. Inajulikana kwa kuwa nchi ya kwanza ya watu weusi kupata uhuru mwaka 1804 baada ya mapinduzi dhidi ya utawala wa Kifaransa, na kwa historia yake tajiri ya kiutamaduni, pamoja na changamoto za kisiasa na za majanga ya asili kama vile matetemeko ya ardhi.

Ukweli wa haraka Jamhuri ya Haiti République d'Haïti (Kifaransa), Repiblik d Ayiti (Krioli ya Kihaiti), Lugha rasmi ...
Thumb
Ramani ya Haiti

Haiti ina historia ya kipekee inayohusisha mapambano ya muda mrefu ya uhuru, ukoloni, na mabadiliko ya kijamii. Baada ya kuongoza mapinduzi ya watumwa yaliyofanikiwa dhidi ya Ufaransa, Haiti ikawa taifa la kwanza la watu weusi kujitawala, jambo lililokuwa na athari kubwa duniani kote. Hata hivyo, tangu wakati huo nchi imekumbwa na mfululizo wa matatizo ya kisiasa, mapinduzi ya kijeshi, na ukosefu wa uthabiti wa serikali, hali ambayo imeathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Katika karne ya 21, Haiti imekumbwa na majanga kadhaa ya asili, ikiwa ni pamoja na tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2010 lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000 na kuacha mamilioni bila makazi. Mifumo ya afya, elimu na miundombinu imeendelea kuwa dhaifu, huku uchumi ukitegemea misaada ya kimataifa, uhamishaji wa fedha kutoka kwa watu waishio nje ya nchi, na sekta ndogo ya kilimo. Licha ya hayo, watu wa Haiti wanaonyesha uthabiti mkubwa, wakihifadhi tamaduni zao tajiri, muziki, sanaa, na lugha yao ya Krioli ya Haiti.

Remove ads

Jiografia

Jina la "Haiti" lina asili katika lugha ya Kitaino ya wakazi asilia; linamaanisha "nchi ya milima", na kweli kisiwa kina milima mingi.

Nchi imegawanywa katika wilaya kumi.

Historia

Mwanzo na ukoloni wa Hispania

Wakazi asilia walikuwa Waindio Waarawak.

Baada ya kufika kwa Kristoforo Kolumbus na utawala wa Hispania idadi yao ilipungua haraka kutokana na magonjwa ya Ulaya ambayo hawakuzoea na kukosa kinga dhidi yake, lakini pia kutokana na kutendwa kwa unyama na mabwana wapya.

Wahispania walianzisha mashamba kwa kutegemea kazi ya watumwa kutoka Afrika.

Mnamo mwaka 1600 Waindio wachache tu walibaki kutoka malakhi wakati wa Kolumbus wakapotea kabisa kwa njia ya kuoa au kuolewa na Wazungu na Waafrika.

Ukoloni wa Ufaransa

Katika karne ya 17 Wafaransa walifika kisiwani wakanunua theluthi moja ya kisiwa wakaiita "Saint-Domingue" kilichokuwa baadaye Haiti. Wafaransa walileta watumwa wengi kutoka Afrika na kujenga uchumi wa mashamba makubwa, hasa ya miwa. Koloni la Saint-Domingue lilikuwa koloni tajiri la Ufaransa katika Amerika.

Mapinduzi ya Ufaransa

Wakati wa mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 koloni lilikuwa na wakazi wa aina nne:

  • Wazungu, hasa Wafaransa, waliokuwa mabwana lakini walikuwa na tofauti kubwa kati yao: wengine tajiri sana wengine maskini - jumla takriban watu 32,000
  • machotara na Weusi huru ambao walikuwa raia wa daraja ya pili; wengine walikuwa matajiri na mabwana wa mashamba na pia wa watumwa - jumla watu 28,000
  • watumwa wenye asili ya Kiafrika - jumla watu 500,000
  • Wamaroni walikuwa watumwa wakimbizi walioishi mlimani katika pori - idadi yao haijulikani lakini hawakuwa wengi.

Mapinduzi ya Ufaransa na kutangaziwa kwa haki za kibinadamu vilisababisha matumaini ya machotara wenye mali ya kukubaliwa kama raia kamili wenye haki ya kupiga kura. Wenyewe hawakutegemea kumaliza utumwa uliokuwa msingi wa uchumi. Lakini matumaini yao yalishindikana wakakataliwa na watawala kisiwani.

Thumb
Toussaint L'Ouverture kiongozi wa uhuru wa Haiti

Mapinduzi ya Haiti

Sehemu ya matajiri kati ya Wazungu walitaka kujitenga na Ufaransa kwa msaada wa Uingereza na Hispania wakichukia mapinduzi katika Ufaransa. Watumwa na Weusi huru wenye elimu walifuata habari hizi wakaogopa ya kwamba utawala wa mabwana hao bila sheria za Ufaransa utakuwa mbaya kuliko hali jinsi ilivyokuwa wakaanza mapinduzi.

Kiongozi wao alikuwa Toussaint L'Ouverture aliyefaulu kushika serikali ya koloni tangu mwaka 1798. Awali alipigania jeshi la Ufaransa; baada ya bunge la Paris kutangaza mwisho wa utumwa alishirikiana na Ufaransa dhidi ya jeshi la mabwana wenye mashamba waliotaka kuendeleza utumwa katika nchi ya kujitegemea.

Toussaint L'Ouverture alishinda pia Waingereza waliotaka kuwasaidia wapinzani Wafaransa wa Paris na mwaka 1801 akateka kaskazini mwa kisiwa iliyokuwa eneo la Kihispania na kutawala Hispaniola yote akitangaza kote mwisho wa utumwa.

Lakini mnamo mwaka 1802 siasa ya Paris ilibadilika na mtawala Napoleon Bonaparte aliamua kurudisha Hispaniola katika hali ya awali akatuma jeshi kubwa la askari 40,000. L'Ouverture alikamatwa alipokubali kushauriana na jenerali Mfaransa akapelekwa kama mfungwa Ulaya. Lakini makamu wake Jean-Jacques Dessalines aliposikia kuhusu mipango ya Ufaransa ya kurudisha utumwa alianza vita upya. Katika vita vikali Wafaransa walishindwa na Dessalines alitangaza uhuru wa koloni tarehe 1 Januari 1804 kwa jina la "Haiti" kama "Jamhuri ya watu weusi".

Remove ads

Wilaya za Haiti

Thumb
Wilaya za Haiti
Thumb
MINUSTAH kazini wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2006.
  1. Artibonite (Gonaïves)
  2. Centre (Hinche)
  3. Grand'Anse (Jérémie)
  4. Nippes (Miragoâne)
  5. Nord (Cap-Haïtien)
  6. Nord-Est (Fort-Liberté)
  7. Nord-Ouest (Port-de-Paix)
  8. Ouest (Port-au-Prince)
  9. Sud-Est (Jacmel)
  10. Sud (Les Cayes)

Watu

Wakazi ni 11,439.646 (2018), lakini wananchi wengine wengi wamehama kutokana na ufukara. Karibu 900,000 wako Marekani, 800,000 wako Dominikana na 300,000 Kuba, halafu Kanada, Ufaransa, Bahamas.

Uchunguzi wa DNA umeonyesha kwamba Afrika Kusini kwa Sahara imeichangia 95.5% na Ulaya 4.3%.

Kuna lugha rasmi mbili: moja ni Kifaransa (42%) na nyingine ni Kihaiti ("Kreyol") inayotokana nacho (karibu 100%).

Wakazi wengi ni wafuasi wa Yesu Kristo (86.4%) (katika Kanisa Katoliki 56.8% na madhehebu ya Kiprotestanti 29.6%) lakini wengi hufuata vilevile dini ya vudu inayotokana na dini za jadi kutoka Afrika ya Magharibi.

Remove ads

Tazama pia

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu maeneo ya Bahari ya Karibi bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Haiti kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Remove ads
Loading related searches...

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Remove ads