Wakoleta

From Wikipedia, the free encyclopedia

Remove ads

Wakoleta ni jina la watawa wa mashirika ya Fransisko wa Asizi waliofuata urekebisho ulioletwa na Koleta Boylet [1].

Bikira huyo, kisha kuishi utawani sehemu mbalimbali, akichukia ulegevu uliotawala huko, alijifungia upwekeni katika nyumba ndogo karibu na kanisa (1402-1406), halafu alitokewa mara kadhaa na Fransisko na kuhimizwa arekebishe utawa wake hata akajiunga na Wafransisko kwa kuvaa mavazi ya Wafransisko Wasekulari.

Mara akaenda kwa Papa wa Avinyon, antipapa Benedikto XIII (bila ya kutambua kwamba ni bandia), akaweka mikononi mwake nadhiri ya kushika mtindo wa maisha wa Klara, akafanywa naye abesi na mrekebishaji wa utawa wote wa Fransisko (I-II-III), kutokana na karama yake wazi ya kurekebisha Kanisa kuanzia monasteri na miundo mingine ya Kifransisko ili vifuate upya ufukara na toba kama walivyofanya na kutaka Fransisko na Klara.

Kwa neema ya Mungu na kwa msaada wa wakuu wa dunia akaanza kutembelea Ufaransa na Benelux ili kueneza chachu ya Kiinjili, hasa ufukara. Upande wa Waklara alirekebisha au kuanzisha monasteri 22 kufuatana na kanuni I aliyoomba nakala yake halisi kwa monasteri mama ya Asizi. Mwenyewe aliiongezea katiba iliyopitishwa na Mtumishi mkuu wa Ndugu Wadogo (1432) halafu ikathibitishwa na Papa Pius II (1458-1464).

Humo alikataza mahari za masista, mali yoyote na mapato ya hakika kwa monasteri, kodi na ghala za kutosha muda mrefu, kila kitu cha thamani au kisicho cha lazima, majengo yasiyo duni. Aliagiza wote wafanye kazi ili kupata riziki, bila ya kuagiza watu wa nje kwa kazi wanazoweza kuzifanya wenyewe. Kwa udogo, alikataza baraka kuu kwa abesi na ibada ya kuweka wakfu mabikira. Hata hivyo alisisitiza usafi na masomo na kupunguza masharti ya ugo. Kwa ajili ya upendo wa kidugu alifuta matabaka, aliagiza vipindi vya burudani (maongezi), alisisitiza mikutano ya kila wiki, alionyesha tena kuwa wadhifa wowote ni utumishi tu. Ingawa alikubali vipengele kadhaa vya kanuni ya Urbani IV vilivyopata kuwa vya kawaida, kwa jumla alirudia vizuri karama ya Klara. Kama yeye alitaka mafungamano imara na Utawa I, monasteri zote zikiwa chini ya Ndugu Wadogo, na wanne kati yao wakiwa tayari kuihudumia kila mojawapo [2].

Remove ads

Ndugu Wadogo Wakoleta

Kwa sababu hiyo watawa kadhaa wa kiume waliingia katika juhudi zake za urekebisho (Ndugu Wadogo Wakoleta) mwaka 1410 hivi. Hao walikubaliwa kama tawi la kujitegemea ndani ya shirika tarehe 11 Septemba 1427 [3] hadi walipounganishwa na Waoservanti mwaka 1517 kwa hati ya Papa Leo X Ite et vos ya tarehe 29 Mei 1517. [4]

Takwimu

Mwishoni mwa mwaka 2005 Waklara Wakoleta walikuwa 668 katika monasteri 57.[5]

Tanbihi

Marejeo

Loading related searches...

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Remove ads