From Wikipedia, the free encyclopedia
Historia ya Mali inahusu eneo la Afrika Magharibi ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Mali.
Mali ina historia ndefu ambayo ni historia ya pamoja ya nchi za kanda la Sahel na kanda la Sudan.
Zamani za Wafinisia na za Waroma palikuwa na mawasiliano ya biashara na nchi za Mediteranea kupitia wanafayabiashara Waberberi walioelewa njia za Sahara.
Uvamizi wa Wavandali katika Afrika ya Kaskazini ulivuruga mawasiliano hayo.
Baada ya uvamizi wa Waarabu na uenezaji wa Uislamu biashara ilianza upya. Ndio Waberberi Waislamu walioingiza dini mpya hata kusini ya Sahara.
Katika eneo la Mali ya leo pamoja na nchi jirani ni hasa madola matatu makubwa yaliyotawala upande wa kusini wa njia za biashara iliyovuka Sahara.
Dola la kwanza lilikuwa Dola la Ghana. Kuanzia karne ya 8 BK hadi mwaka 1076 lilitawala biashara ya dhahabu, pembe za ndovu na chumvi. Mji mkuu ulikuwa Kumbi Sale wenye wakazi 30,000 katika Mauretania ya leo.
Taarifa za wanahistoria Waarabu zimeonyesha ufalme tajiri. Utamaduni wake haukuwa wa Kiislamu bali wa Kiafrika asilia.
Mwisho wake ulianza wakati jeshi la Wamurabitun kutoka Moroko lilivuka jangwa na kuvamia Kumbi Sale.
Mali ilianza kama ufalme mdogo wa Wamalinke kando ya Ghana. Wakati wa karne ya 13 ilianza kupanuka chini ya mfalme Sundiata Keita. Sundiata mwenyewe alipokea Uislamu mnamo 1240 BK na wafalme baada yake waliendela kuwa Waislamu.
Mfalme wa Mali aliyejulikana zaidi ndiye Mansa Kankan Musa I (1312–1337). Miaka 1324-1325 alihiji kwenda Makka. Alisafiri na dhahabu nyingi sana. Huku Misri alitoa zawadi kiasi cha kuharibu thamani ya dhahabu kwa miaka 12 iliyofuata.
Wakati ule mji wa Timbuktu ulikuwa kitovu cha biashara na elimu iliyojulikana kote katika umma wa Kiislamu hata Ulaya.
Katika karne ya 14 BK uwezo na utawala wa Mali ulipungua na Songhai ilichukua nafasi yake.
Asili ya Wasonghai ilikuwa Nigeria ya Kaskazini ya leo. Walipanua utawala wao kuelekea magharibi wakapokea Uislamu wakati wa uvamizi wa Almurabitun.
Mnamo mwaka 1250 walikuwa chini ya Mali lakini katika karne ya 14 walijipatia uhuru tena, wakaanza kushika maeneo ya Mali yenyewe.
Kilele cha nguvu yake ilikuwa wakati wa mfalme Askia Mohammad I katika karne ya 16 walipotawala eneo kubwa kutoka Kano (Nigeria) hadi pwani ya Atlantiki. Wakati wake mji wa Timbuktu ilitembelewa na msafiri Leo Africanus aliyeleta baadaye habari za nchi hadi Ulaya.
Utawala wao uliporomoka baada ya mashumbulizi kutoka Moroko mwaka 1591. Wakati ule mataifa ya Ulaya yameshaanza kufika kwenye mwambao wa Afrika ya Magharibi wakifungua biashara ya moja kwa moja na Ulaya. Umuhimu wa biashara ya kuvuka Sahara ulipungua vikali pamoja na faida iliyopatikana kwa watawala katika maeneo ya Sahel.
Kilichofuata kilikuwa kipindi cha madola madogo. Viongozi Waislamu walijaribu mara kadhaa kujenga utawala juu ya eneo lote.
Anayejulikana zaidi alikuwa Alhaj Omar aliyepiga vita kwa jina la dini ya Kiislamu dhidi ya Wabambara waliofuata utamaduni na dini asilia za Kiafrika.
Mtoto wa Alhaj Omar aliyeitwa Ahmadu alijaribu kuendeleza jihadi yake. Lakini wakati ule Wafaransa walianza kuenea katika Afrika ya Magharibi wakamshinda.
Mali ikawa koloni la Ufaransa kuanzia mwaka 1895. Ilikuwa sehemu ya Afrika ya Magharibi ya Kifaransa, na kuanzia 1920 ya Sudan ya Kifaransa.
Mwaka 1960 Mali pamoja na Senegal zilipata uhuru kama "Shirikisho la Mali". Baada ya Senegal kuacha umoja huo, Jamhuri ya Mali chini ya rais wa kwanza Modibo Keïta ikawa nchi ya kujitegemea.
Keita alipinduliwa mwaka 1968 na wanajeshi akishtakiwa kuwa ameharibu uchumi na kujitajirisha. Kiongozi mpya Moussa Traoré alitawala kama dikteta wa kijeshi, baadaye kwa msaada wa katiba ya chama kimoja.
Mabadiliko yaliyotokea kote Afrika tangu mwisho wa Ukomunisti kuanzia miaka ya 1990 yalisababisha kupinduliwa kwa Traoré katika Machi 1991 na kamati ya kijeshi iliyoongozwa na Amadou Toumani Touré.
Katiba mpya ya mwaka 1992 iliunda kipindi cha kura huru alimoshinda Amadou.
Mnamo Septemba 2021, mkataba ulisainiwa kati ya serikali ya Mali na kampuni binafsi ya jeshi la Urusi iliyounganishwa na kikundi cha jeshi la Urusi Wagner. Hati hiyo inataka kupelekwa kwa mamluki nchini, kwa kushirikiana na jeshi la Mali, na ulinzi wa wahusika wakuu.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.