Ufalme
From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Ufalme ni mfumo wa utawala ambapo mfalme, malkia au mtu mwingine aliyerithi cheo chake ni mkuu wa dola. Vyeo vingine vya mkuu katika ufalme ni pamoja na kaisari, shah, tenno, sultani, amiri au mtemi. Kwa kawaida mfalme amerithi cheo chake kutoka kwa baba yake au mama yake, kwa hiyo alizaliwa kama mfalme mteule na ataendelea kuwa na cheo hicho hadi kifo chake. Lakini kama mfalme aliyetangulia hakuwa na mrithi inawezekana ya kwamba mfalme mpya amechaguliwa. Mfano wa dola lenye mfumo wa ufalme ambapo mkuu anachaguliwa mara kwa mara ni Vatikani ambapo Papa ni mkuu wa dola.

Neno ufalme hutumiwa pia kwa kutaja nchi inayotawaliwa na mfalme au malkia, kwa mfano Ufalme wa Maungano, Ufalme wa Eswatini na kadhalika.
Kiwango cha madaraka cha mfalme huwa na tofauti kubwa. Leo hii wafalme wengi wako chini ya katiba ya nchi na mara nyingi wana madaraka machache; nafasi yao ni ya heshima na desturi. Lakini kuna falme kadhaa ambaPo mfalme bado ana madaraka makubwa, habanwi na katiba wala bunge wala serikali kama vile Omani au Saudia.
Remove ads
Tofauti ya ufalme na jamhuri
Kinyume cha ufalme ni jamhuri inayoongozwa na mkuu, mara nyingi kwa cheo cha rais au katika nchi kadhaa na kamati ya watu wanaochaguliwa na kwa kawaida kwa kipindi fulani. Mara nyingi rais wa nchi huchaguliwa kwa kipindi cha miaka 4-6 na katika nchi nyingi kuna uwezekano Wa kwamba anarudi tena kwa kipindi kingine. Kuna jamhuri ambapo vongozi wanalenga kuhakikisha ya kwamba mtoto wao anaendelea na cheo cha mkuu wakiacha kutawala, lakini hii kwa kawaida si utaratibu wa kisheria katika jamhuri; mfano wa kisasa ni Korea Kaskazini ambayo ni jamhuri inayotawaliwa na familia Kim katika kizazi cha pili ilhali mtoto wa kiongozi Kim Jong Il anateuliwa kumfuata baba.
Remove ads
Historia
Sababu za kuanzishwa kwa ufalme
Ufalme ni muundo wa kale sana lakini haukuwa mfumo wa kwanza wa serikali. Wataalamu huona ya kwamba chanzo chake ni azimio la kabila au kundi dogo la watu kumruhusu mtoto wa kiongozi mwenye nguvu na uwezo kuendelea na shughuli za baba. Kuna mifano watu walioishi na viongozi wa muda tu waliamua kuwa na mfalme wakati wa vita wakiona uongozi wenye nguvu ni wa lazima. Kulitokea pia ya kwamba kiongozi aliyeteuliwa kwa kipindi cha matatizo au vita alionekana kuwa na uwezo akaendelea hadi kifo na kumpatia mtoto wake nafasi ya mrithi wakati alipokuwa bado na nguvu.
Historia ya Biblia kama mfano wa kuanzishwa kwa ufalme
Biblia inasimulia jinsi gani watu wa Israeli ya Kale walioongozwa kila mahali na wazee lakini kama walipata matatizo makubwa viongozi walijitokeza walioitwa "Waamuzi" na kuwa na majukumu ya kijeshi pamoja na ya kisheria. Kitabu cha Waamuzi 8#22 kinaonyesha pia jinsi gani suala la ufalme lilivyokuwa na ugumu; mwamuzi Gideon alipoombwa na watu kuwa mfalme alikataa na kudokeza ya kwamba Mungu pekee anastahili kuwa na cheo hicho. Baadaye Sauli alijitokeza kama kiongozi dhidi ya tishio la Waamoni; alipowashinda vitani watu walimfanya Sauli mfalme wao wa kwanza. Mataifa mengi walipata ufalme kwa njia zilizofanana na Israeli ya Kale yaani wakati wa vita ambapo wengi walikubali haja ya kiongozi mwenye nguvu.
Kupinduliwa kwa wafalme au kubanwa kwa madaraka yao
Mfano mashuhuri wa kinyume ni historia ya Athens au Roma ya Kale ambazo zilitawaliwa zamani na wafalme lakini viongozi wa miji hiyo walifukuza wafalme baada ya kuona tabia za kidikteta pamoja na kupuuzia haki za watu wakaanzisha jamhuri zilizoteuliwa na viongozi waliochaguliwa kwa muda tu. Lakini Roma ya Kale ilirudia mfumo wa ufalme tangu Kaisari Augusto ingawa kwa jina iliendelea kama jamhuri hadi mwisho.
Mara nyingi wafalme waliunganisha nafasi za mkuu wa serikali na kiongozi wa jeshi na jaji mkuu. Mataifa mbalimbali walimjua mfalme pia katika nafasi ya kidini kama kuhani mkuu au kama mkuu anayeshika nafasi ya Mungu duniani.
Mamlaka kubwa ya wafalme ilisababisha mara nyingi jitihada za kubana madaraka yao. Mfano mashuhuri ni Uingereza ambapo wafalme walipaswa kushauriana na bunge ya wakubwa na wawakilishi wa miji kabla ya kukusanya kodi kwa ajili ya vita au kwa shughuli maalumu. Jambo kama hilo halikutokea katika Uingereza pekee lakini katika nchi hiyo bunge lilikuwa taasisi ya kudumu isiyofutwa tena na hivyo kuwa chanzo cha muundo wa ufalme wa kikatiba ambako mamlaka ya mfalme iko chini ya sheria fulani.
Tangu uhuru wa Uholanzi, Marekani na baadaye mapinduzi ya Kifaransa nafasi ya ufalme ilianza kupungua katika Ulaya na kutoka hapo pia katika sehemu nyingine za dunia. Hasa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia falme muhimu kama Ujerumani, Austria-Hungaria, Urusi na Milki ya Osmani zilibadilisha mfumo wa utawala zikawa jamhuri.
Ukoloni na ufalme
Ukoloni wa karne ya 19 ulisababisha kupotea kwa falme nyingi dunani. Mwanzoni wakoloni walitumia mara nyingi wafalme na watemi waliokuwepo kama mawakala wa utawala wao ndani ya koloni. Lakini kadiri walivyounganisha falme mbalimali za kale ndani ya maeneo mapya makubwa yaliyoendelea kuwa mataifa mapya walidhoofisha pia nafasi ya ufalme wa kieneo.
Nchi za Afrika zilipopata uhuru mara nyingi zilijitangaza kuwa jamhuri na kwa njia hiyo falme za kale za Afrika zilifutwa au kupoteza madaraka ya kiutawala na kubaki kwa jina tu kama taasisi za kiutamaduni.

nyekundu: Ufalme bila masharti ya kikatiba; chungwa: ufalme chini ya masharti kiasi ya kikatiba; kijani: ufalme wa kikatiba; kijani kibichi: nchi za Jumuiya ya Madola chini ya malkia wa Uingereza; dhambarau: ufalme wa kieneo chini ya ngazi ya jamhuri ya kitaifa
Ufalme leo
Kuna nchi 44 duniani zilizoendela na mfumo wa ufalme hadi karne ya 21. (Linganisha jedwali). Ufalme wa kale ni Japani ambapo kuna wafalme tangu zaidi ya miaka 2000. Pia Ufalme wa Muungano, ambao wafalme wanaendelea karibu mfululizo tangu miaka 1,000 hivi, naDenmark tangu miaka 1,200 hivi.
Remove ads
Tanbihi
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads