From Wikipedia, the free encyclopedia
Pembetatu ya Kionga ilikuwa eneo dogo la kilomita za mraba 395 [1] kwenye Bahari ya Hindi, kusini kwa Mto Rovuma na kaskazini mwa Rasi Delgado. Ndani ya eneo hilo kuna mji wa Kionga (kwa Kireno "Quionga"), ambao mwaka wa 1910 ulikuwa na wakazi karibu 4,000.
Eneo hilo lilikuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani lakini tangu mwaka 1918 ni sehemu ya Msumbiji.
Mnamo karne ya 19 eneo karibu na Rasi Delgado lilitawaliwa na Usultani wa Tungi [2], ilhali Ureno ilidai pwani yote hadi Rasi Delgado, lakini haikuwa tena na mamlaka yoyote kaskazini mwa kisiwa cha Ibo. [3] Sultani wake aliishi kwenye Hori ya Tungi, kusini mwa rasi hiyo. Mwaka 1844 mtawala wa Zanzibar Said bin Sultani alikuwa ametangaza kwa Waingereza kwamba himaya yake ilienea hadi Rasi Delgado; lakini mwaka 1848 kutokana na udhaifu wa Ureno alimteua Sultani wa Tungi kuwa gavana, na mwaka 1854 Zanzibar ilimpeleka gavana wake pamoja na kikosi kidogo cha askari kwenda Tungi. [4]
Baada ya kuanzishwa kwa Afrika Mashariki ya Kijerumani mwaka 1885, nguvu ya Zanzibar ilififia. Wakati tume ya kuangalia mipaka ya Ujerumani-Uingereza-Ufaransa iliposafiri ufukweni mwaka 1886 ili kujua ukubwa wa eneo la Wazanzibari, gavana wa Ureno alituma msafara wa kijeshi katika sehemu ya kusini ya Hori ya Tungi, ambapo tume iliamua kuwa eneo la Zanzibar linaenea kusini hadi kwenye mdomo wa Mto Minengani [5] kwenye hori hiyo. [6] . Makubaliano yafuatayo ya mipaka baina YA Uingereza na Ujerumani ya tarehe 29 Oktoba 1886 yalirudia azimio hili, lakini yalitaja eneo la kutenganisha maslahi ya Uingereza na Ujerumani kuwa liliaNza tu kwenye Mto Rovuma. [7]
Kwenye Februari 1887 Wareno walivuka mto Minengani na kuvamia Tungi yenyewe; askari wa Sultani walijiondoa kwenye pwani wakikaa ndani. Serikali ya Sayyid Bargash wa Zanzibar ilipambana wakati uleule na madai ya Waingereza na Wajerumani kuwaachia sehemu za Kizanzibari za pwani za Kenya na Tanganyika za baadaye, hivyo haikuchukua hatua zozote kuwaondoa tena Wareno katika Tungi. Hivyo Wareno waliweza kuimarisha utawala wao hadi Rasi Delgado[8].
Katika makubaliano yafuatayo ya Kijerumani-Kireno ya Desemba 30, 1886, mstari wa Rovuma kutoka mdomoni ulitajwa kuwa mpaka kati ya milki za Wareno na Wajerumani. [9] Ukanda wa pwani bado ulikuwa wa Zanzibar.
Katika Mkataba wa Helgoland-Zanzibar wa mwaka 1890, Ujerumani ilichukua eneo la kusini mwa ukanda wa bara wa Zanzibar katika pwani ya Afrika Mashariki, ingawa maandishi ya mkataba huo yalitaja tu "mpaka wa kaskazini wa jimbo la Msumbiji" na "njia ya mto Rovuma" kama mpaka wa kusini. Kwa hiyo, hali ya eneo la Kizanzibari upande wa kusini mwa Rovuma haikuwa wazi kimkataba.
Upande wa Ujerumani uliamua baadaye kidogo kuchukua udhibiti wa pande zote mbili za mdomo wa mto Rovuma na kumaliza mahali pa Kionga kama bandari ya magendo. [10] Kikosi cha wanamaji cha Ujerumani kilivamia eneo hilo tarehe 16 Juni 1894 na kuanzisha kituo cha Kionga penye ofisi ya forodha. [11] Hatimaye Ureno ilikubali kushiriki katika tume ya pamoja ya mpaka, ambayo mwaka wa 1895 ilikubali mpaka ambao ulipita kaskazini kidogo mwa Rasi Delgado kando ya latitudo 10° 40' hadi Rovuma, ambayo ilifuata kutoka hapa [12]. Hii ilianzisha "pembetatu ya Kionga".
Wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia, Wareno walivamia eneo hadi Mto Rovuma mnamo 1916. [13] Dola la Ujerumani liliwahi kutangaza vita dhidi ya Ureno tarehe 9 Machi 1916. [14]
Tarehe 25 Septemba 1919 katika Mkataba wa Versailles Rovuma hatimaye ilifafanuliwa kama mto wa mpaka hadi mdomoni. Ureno ilipewa pembetatu ya Kionga kama fidia kwa uharibifu wa vita. Azimio kuhusu eneo la Tanganyika lilitambua mto Rovuma kutoka mdomoni hadi kuingia kwa mto Messinge ("M'Sinje") kuwa ni mpaka wa Msumbiji[15].
Pembetatu ya Kionga ilijumuishwa rasmi katika Afrika ya Mashariki ya Kireno kwa sheria n.º 962 tarehe 2 Aprili 1920.
Mamlaka ya Shirikisho la Mataifa na udhamini wa Umoja wa Mataifa baadaye ulimalizika tarehe 25 Juni 1975 wakati wa uhuru wa Msumbiji, ambayo eneo hilo likawa sehemu ya jimbo la Cabo Delgado. [16]
Tarehe 29 Mei 1916 Wareno walitoa stempu za posta za Kionga. Stempu za posta za zamani kutoka koloni la Lourenço Marques (leo Maputo) zilizo na picha ya Mfalme Carlos I na muhuri wa "REPUBLICA" (ufalme wa Ureno ulipinduliwa mwaka wa 1910) zilitumiwa. Kwa kuongeza, neno "Kionga" na thamani mpya ilichapishwa juu yake. Stempu zilithaminiwa kuwa ½, 1, na 2 ½ na 5 centavo. Stemu hizo zinachukuliwa kuwa adimu.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.