Ndugu Bernardo
From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Ndugu Bernardo (karne ya 12 - Assisi, 1245 hivi[1]) alikuwa wa kwanza kati ya wafuasi wa Fransisko wa Asizi akaheshimiwa naye kwa jinsi alivyotekeleza Injili kwa kuwagawia maskini mali zake zote ambazo zilikuwa nyingi[2] mpaka mwisho akamuachia baraka ya pekee.

Maisha
Bernardo, mwana wa Quintavalle wa Berardello, msomi[3] maarufu tena tajiri, halafu Petro Cattani, padri ndio mwanzo wa jamaa ya Ndugu Wadogo iliyokuja kumhangaisha sana Fransisko, kwa sababu hakuwa na wazo la kuanzisha chochote wala hakupata mtu wa kumuelekeza. Tena wakati huo haikuwa rahisi kukubali padri aongozwe na mlei kama yeye.
Katika wasia wake Fransisko akikumbuka hatua hiyo muhimu alisisitiza kuwa ndipo Mungu mwenyewe alipomfunulia afuate mtindo wa Injili takatifu, yaani hasa madondoo yale aliyoyakuta katika kufungua mara tatu kitabu cha Misale kilichokuwa juu ya altare: 1) “Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda ukauze…” 2) “Msichukue chochote kwa safari…” 3) “Anayetaka kunifuata, ajikane…” Baada ya kusoma hayo, aliwaambia wenzake hao wawili ndiyo kanuni na maisha ya wale wote watakaowafuata. Ufukara wa Kifransisko ukifuata madondoo hayo ya Injili ni wa moja kwa moja kwa mtawa binafsi na kwa shirika zima. Kwa kuchagua mtindo huo wa Injili takatifu alitofautiana na watawa wale waliofuata tangu karne nyingi mtindo wa Kanisa la mwanzoni wa kuwa na mali zote shirika. Ndivyo walivyofanya wamonaki ambao hawakuwa na chochote chao binafsi, lakini monasteri zao zilikuwa tajiri, kiasi kwamba wakaanza kushambuliwa kama wanafiki wanaokula jasho la wengine na kukosa ufukara halisi.
Waamini wengi kama Bernardo na padri Petro walitamani mtindo mwingine, pamoja na uadilifu wa makleri, uchungaji wenye bidii na ujirani na watu, hasa wenye shida. Mungu aliwachagua watakatifu Fransisko na Dominiko Guzman ili kuridhisha Wakristo hao. Wote wawili walishika ufukara wa kijumuia pia, ingawa Mt. Fransisko aliusisitiza zaidi akiudai pia kama msimamo katika jamii ili kupigania ujamaa na usawa wa binadamu. Hata baada ya wengine kujiunga naye hakushughulikia suala la nyumba: waliishi kwenye pagale za makanisa, huku wakizungumziwa sana mjini kwao. Halafu wakaanza kusafiri wakihubiri huko na huko, si kama kawaida ya mapadri, bali kwa kutoa mfano wa ufukara na unyenyekevu, halafu kwa kujibu maswali ya watu waliowashangaa. Polepole waliweza pia kuhimiza toba na msamaha ili kueneza amani: muhtasari wa mawaidha yao ni salamu ile ambayo Fransisko alidai kufunuliwa na Mungu, “Bwana akujalie amani”.
Baada ya jaribio la kwanza la namna hiyo wakaongezeka, naye akawatuma tena wawiliwawili sehemu mbalimbali kisha kuwashirikisha mang’amuzi yake, kwamba wasikate tamaa kwa kuona ugumu wa baadhi ya watu, wamtegemee Mungu, wahubiri toba kwa nguvu ili kuokoa watu, wadumu watulivu katika dharau. Walipoulizwa waitwaje walijibu tu kuwa ni watu wa toba kutoka Asizi, yaani hawakujiona kuwa shirika maalumu, bali kundi mojawapo la wale wengi ambao toka zamani walijifunga kufanya toba kwa namna maalumu hadharani.
Mwaka huohuo (1209) walipofikia idadi ya 12 walichukua hatua ya kuelekea Roma ili kuthibitishwa na Papa katika maisha yao na kuruhusiwa naye katika utume wao, ili kushinda upinzani uliojitokeza na hasa kujihakikishia njia yao ni njema. Kwa ajili hiyo walipaswa kupanga kikamilifu zaidi wanataka kufanya nini.
Kisha kukubaliwa, walirudi kwa furaha Asizi walibanana katika kibanda fulani huko Rivotorto, halafu wakahamia Porsyunkula. Mahali penyewe panasaidia sana kuelewa karama ya Kifransisko: si maisha ya kimonaki yanayohitaji kujitegemea kwa mashamba makubwa na mifugo, wala ya wakaapweke wanaohitaji kuishi mbali na watu, bali ni utawa unaohitaji utulivu na upweke kwa ajili ya sala, lakini pia unadai uhusiano mkubwa na watu wa nje ili kupata riziki na hasa kuwajenga kwa mifano na maneno. Hivyo si kati ya watu, wala si mbali nao.
Mchana ndugu walikuwa wakienda mjini kufanya kazi mbalimbali ndogondogo na kuwahimiza watu waishi kwa uadilifu. Muda uliobaki, hasa usiku, ulikuwa kwa ajili ya sala upwekeni. Maelezo mengine kuhusu maisha ya wakati huo tunayapata tena katika wasia ambamo Fransisko ametuachia ukumbusho wa kudumu.
Baadaye Bernardo alipelekwa Bologna, ila alipoanza kuheshimiwa na wananchi aliomba kuhama asije akapatwa na kiburi[4], akaenda Lombardia[5].
Mwaka 1212 alitumwa kumhamisha Klara kutoka monasteri moja hadi nyingine ya Wabenedikto wa kike ili apate ulinzi kamili zaidi dhidi ya familia iliyotaka kumrudisha nyumbani.
Kati ya miaka 1213 na 1214 aliongozana na Fransisko hadi Hispania katika jaribio la kwenda kuwahubiria Waislamu wa Moroko.
Baadaye akawa mtumishi wa kanda Hispania hadi mwaka 1219[6]. Ndipo aliporudi Italia akawa jirani na Fransisko katika miaka yake ya maradhi na mateso makali zaidi.
Siku za mwisho za Fransisko zilijaa ishara za upendo kwa marafiki wake: njiani alibariki Asizi na kuuombea, akamtabiria Klara kuwa atamuona na kufarijika, akawaita ndugu waliokuwa mbali (hata “kaka” Yakopa wa Settesoli kutoka Roma), akawagawia vipande vya mkate akifuata mfano wa Yesu. Katika yote alilenga ustawi wa roho zao na wa shirika, tunavyoona hasa katika baraka zake za mwisho alizozitoa kwa kufuata mfano wa mababu wa Israeli na Musa. Aliwabariki waliokuwepo na kwa njia yao alikusudia kuwabariki wale wote watakaoingia shirikani mpaka mwisho wa dunia.
Kati ya wote ndugu Bernardo alipata baraka ya pekee akaandikiwa maneno yafuatayo yawe kumbukumbu kwa wote siku za mbele: “Ndugu wa kwanza aliyenipa Bwana ni ndugu Bernardo, naye ndiye wa kwanza kutekeleza kikamilifu kabisa Injili takatifu akiwagawia maskini mali zake zote. Kwa hiyo na kwa sifa nyingine nyingi napaswa kumpendelea kuliko ndugu mwingine yeyote katika shirika zima. Ndiyo sababu nataka na kuagiza kadiri ninavyoweza kwamba yeyote atakayekuwa mtumishi mkuu ampende na kumheshimu kama nafsi yangu, na vilevile watumishi wengine wa kanda na ndugu wa shirika lote wamjali kama ni mimi mwenyewe”. Ndiyo mbinu ya mwisho ya Fransisko ili kuzuia utawa wake usipotoke: kumuacha mtu ambaye awe kielelezo kwa viongozi na kwa ndugu wengine badala ya mwanzilishi. Kisha kumuacha huyo mwandamizi (si katika uongozi bali katika kazi muhimu zaidi ya kuwa kielelezo), Fransisko hatimaye aliweza kuaga dunia amemaliza kazi yake na kulazwa uchi ardhini, usiku kati ya tarehe 3 na 4 Oktoba 1226.
Akitegemea agizo hilo la Fransisko, Bernardo alithubutu kumlaumu Elia, mtumishi mkuu, kwa jinsi alivyoishi kwa fahari kinyume cha kanuni ya Ndugu Wadogo[6].
Mbali ya tukio hilo, Bernardo aliishi miaka yake ya mwisho upwekeni hadi alipofariki dunia.
Kaburi lake linakabiliana na lile la Fransisko chini ya altare ya Basilika lake[7].
Remove ads
Tanbihi
Marejeo
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads