Porsyunkula
From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Porsyunkula (kwa Kiitalia Porziuncola, kutoka jina la Kilatini Portiuncula, lenye maana ya "Kasehemu") ni kikanisa cha zamani katika bonde linaloenea chini ya mji wa Assisi ambalo lilipata umaarufu kutokana na Fransisko wa Asizi kuishi na kufariki huko.


Kwa sasa kikanisa hicho, chenye urefu wa mita 5.5 na upana wa mita 3.2, kinapatikana ndani ya basilika la Kipapa linalotembelewa na mamilioni ya watu kila mwaka.
Remove ads
Historia
Mwaka 1209, kisha kurudi kwa furaha toka Roma walipopata kibali cha Papa Inosenti III, kwanza walibanana katika kibanda fulani huko Rivotorto, halafu wakahamia Porsyunkula, mahali pa kikanisa ambacho kilijengwa kwa heshima ya Bikira Maria wa Malaika na ambacho Fransisko alikuwa amekikarabati miaka ya kwanza baada ya uongofu wake [1]. Miaka hiyo ilikuwa migumu sana kimwili na kiroho tukizingatia pia mahangaiko yake kuhusu wito.
Mahali penyewe panatusaidia sana kuelewa karama ya Kifransisko: si maisha ya kimonaki yanayohitaji kujitegemea kwa mashamba makubwa na mifugo, wala ya wakaapweke wanaohitaji kuishi mbali na watu, bali ni utawa unaohitaji utulivu na upweke kwa ajili ya sala, lakini pia unadai uhusiano mkubwa na watu wa nje ili kupata riziki na hasa kuwajenga kwa mifano na maneno. Hivyo si kati ya watu, wala si mbali nao (kilomita 2-3).
Mchana ndugu walikuwa wakienda mjini kufanya kazi mbalimbali ndogondogo na kuwahimiza watu waishi kwa uadilifu. Muda uliobaki, hasa usiku, ulikuwa kwa ajili ya sala upwekeni. Maelezo mengine kuhusu maisha ya wakati huo tunayapata tena katika wasia ambamo Fransisko ametuachia ukumbusho wa kudumu.
Mwaka 1211 Wabenedikto, waliomiliki kikanisa hicho, walimkodisha Fransisko kwa sharti la kwamba kiwe nyumba mama ya shirika lake jipya. Kweli, mikutano mikuu ya kwanza ya shirika ilifanyika huko.
Mwaka 1212 Fransisko alimpokea huko Klara, mwanamke wa kwanza kuwa mfuasi wake, na kumweka wakfu kwa Mungu kwa kumnyoa kitawa.
Kutoka Porsyunkula Fransisko aliendelea kusafiri hasa kwa ajili ya utume uliomfikisha hadi Mashariki ya Kati (1219-1220) lakini kila mara alirudi. Miaka ya mwisho safari zake zilizidi kupungua kwa wingi na kwa umbali, zikifanyika hasa kwa kujaribu matibabu ya maradhi yake makubwa.
Hata katika hali hiyo Fransisko hakuacha kulihangaikia shirika lake kadiri alivyoona linasogea mbali na karama yake. Ili awe kielelezo kwa wote alizidi kujinyima mahitaji ya mwili, na kutamani arudie maisha yaliyodharauliwa ya mwanzoni na kutumikia wakoma. Ndipo alipowaambia wenzake, “Ndugu, tuanze kumtumikia Bwana Mungu, kwa kuwa mpaka sasa hatujapiga hatua au ni ndogo sana”.
Aliogopa shirika lake litalegea kama mengine mengi, hivyo akatafuta mbinu za kuliokoa, kusudi kanuni isiwe mwisho wa juhudi za ndugu, bali kichocheo kwa kutafuta ukamilifu. Mbinu mojawapo ni wasia wa Kiroho aliouandika zaidi ya mara moja. Muhimu zaidi ni ule mrefu aliouandika katika wiki za mwisho za maisha yake. Haukukusudiwa kuwa kanuni mpya, ila kusaidia ile iliyoahidiwa kwa Bwana: ni kumbukumbu, onyo na shauri.
Mbali ya maandishi yake, Fransisko alitafuta mbinu nyingine ili kudumisha shirika katika karama yake. Mojawapo ni kuwaagiza watumishi wa shirika watunze Porsyunkula kama kielelezo cha ufukara, kimya na sala ili ndugu wote wakumbuke wanavyopaswa kuishi. Kwa ajili hiyo alitaka wapangwe huko ndugu bora ambao mmojawao akifa, nafasi yake ishikwe na mwingine. Hivyo alisisitiza tena umuhimu wa mifano, ambayo isiwe ya mtu mmojammoja tu, bali ya jumuia nzima pia. Jambo hilo halikutekelezwa mahali pale, lakini katika historia ya shirika tunaona daima ndugu wakiomba ruhusa ya kutekeleza kikamilifu kanuni pamoja na wengine, hasa katika makao ya upwekeni; tunaona pia mchango mkubwa wa jumuia hizo katika kurekebisha kwa mfano wao hali ya utawa mzima. Mfransisko ni ndugu hasa, na maisha yake yanategemea sana jumuia: hawezi kuridhika ashike kanuni kibinafsi katika jumuia iliyolegea; ndiyo sababu ya maombi hayo. Pengine viongozi wenyewe wa shirika walipoona limelegea mno wakaja kuhamasisha wenye nia waunde jumuia za pekee. Namna zote mbili zikazaa matunda tele.
Fransisko, baaada ya kuuguzwa katika jumba la Askofu wa Asizi kwa siku kadhaa, aliomba ahamishiwe Porsyunkula ili afie pale alipoanzia maisha mapya. Alikuwa amebaki mifupa na ngozi tu, isipokuwa tumbo na miguu vimevimba kama kwa safura. Ndipo alipotunga ubeti wa mwisho wa Utenzi wa Viumbe Vyote. Mwaka mmoja kabla ya hapo alikwishaongeza ubeti mwingine juu ya msamaha ili kuwapatanisha Askofu na Meya wa Asizi. Basi ubeti juu ya kifo ukaja kukamilisha utenzi mzima kwa kuchungulia uzima wa milele, ambapo sifa za Mungu zinaimbwa bila mwisho. Ndivyo alivyojiandaa kufa katika mapenzi ya Mungu.
Siku za mwisho zilijaa ishara za upendo kwa marafiki wake: njiani alibariki Asizi na kuuombea, akamtabiria Klara kuwa atamuona na kufarijika, akawaita ndugu waliokuwa mbali (hata “kaka” Yakopa wa Settesoli kutoka Roma), akawagawia vipande vya mkate akifuata mfano wa Yesu. Katika yote alilenga ustawi wa roho zao na wa shirika, tunavyoona hasa katika baraka zake za mwisho alizozitoa kwa kufuata mfano wa mababu wa Israeli na Musa. Aliwabariki waliokuwepo na kwa njia yao alikusudia kuwabariki wale wote watakaoingia shirikani mpaka mwisho wa dunia.
Kati ya wote ndugu Bernardo alipata baraka ya pekee akaandikiwa maneno yafuatayo yawe kumbukumbu kwa wote siku za mbele: “Ndugu wa kwanza aliyenipa Bwana ni ndugu Bernardo, naye ndiye wa kwanza kutekeleza kikamilifu kabisa Injili takatifu akiwagawia maskini mali zake zote. Kwa hiyo na kwa sifa nyingine nyingi napaswa kumpendelea kuliko ndugu mwingine yeyote katika shirika zima. Ndiyo sababu nataka na kuagiza kadiri ninavyoweza kwamba yeyote atakayekuwa mtumishi mkuu ampende na kumheshimu kama nafsi yangu, na vilevile watumishi wengine wa kanda na ndugu wa shirika lote wamjali kama ni mimi mwenyewe”. Ndiyo mbinu ya mwisho ya Fransisko ili kuzuia utawa wake usipotoke: kumuacha mtu ambaye awe kielelezo kwa viongozi na kwa ndugu wengine badala ya mwanzilishi.
Kisha kumuacha huyo mwandamizi (si katika uongozi bali katika kazi muhimu zaidi ya kuwa kielelezo), Fransisko hatimaye aliweza kuaga dunia amemaliza kazi yake na kulazwa uchi ardhini. Mauti, ambayo yeye alipenda kuiita ndugu, ilimfikia huko usiku wa kuamkia tarehe 4 Oktoba.
Remove ads
Tanbihi
Marejeo
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads