Waklareno

From Wikipedia, the free encyclopedia

Waklareno

Waklareno walikuwa watawa wa shirika la Ndugu Wadogo ambao katika Karne za Kati walipigania kushika kanuni iliyoandikwa na Fransisko wa Asizi bila kujali ufafanuzi wake.

Thumb
Kitabu cha Nyaraka za Angelo Klareno.

Historia

Wafransisko wa namna hiyo walijulikana kwanza kama "Watu wa Kiroho" kwa sababu walitaka kufuata kanuni hiyo "kadiri ya Roho Mtakatifu" tu. Hao ndugu walishikilia ufukara kiasi cha kushindana na viongozi wa shirika na wa Kanisa Katoliki[1]. Hatimaye mambo yakawa magumu kiasi kwamba suala hilo likawa zito kwa Kanisa lote.

Ni kwamba, wakati wa Mtaguso wa pili wa Lyon, baadhi ya ndugu hao walijiandaa kukataa maagizo waliyoambiwa watapewa kinyume cha haki. Upinzani wao ukalipuka hasa baada ya Papa Nikola III (1277-1280) kutoa hati nyingine juu ya kanuni (1279) ili kuwaondolea Ndugu Wadogo wasiwasi wowote kuhusu namna ya kuitekeleza, pamoja na kuwatetea dhidi ya maadui wa nje.

Hati hiyo inafuata kabisa msimamo wa Bonaventura wa Bagnoregio kuhusu matumizi ya kifukara kweli: Ndugu Wadogo hawana haki ya kutumia vitu, ila wanaruhusiwa kuvitumia kadiri ya ufukara na uduni.

Ingawa hati hiyo ilitungwa kwa busara sana, baada ya kamati kabambe kuiandaa kwa miezi miwili, utekelezaji wake ukaja kusababisha mabishano makubwa kwa miaka mingi, kuanzia Ufaransa Kusini na Italia ya Kati.

Mwakilishi bora wa msimamo mkali ni Petro wa Yohane Olivi (1248-1298), aliyeunganisha pande hizo mbili tofauti: wa kwanza ulitegemea ujuzi mkubwa ukaathiri zaidi Kanisa kwa ufundishaji, uchungaji na uanzishaji wa jumuia za waamini zilizowaunga mkono; wa pili ulitegemea zaidi kumbukumbu chungu za wenzi wa Fransisko wa Asizi na matabiri juu ya dhuluma utawani ukaishia kuathiri shirika (hata kwa utunzi wa vitabu muhimu, hasa cha Ubertino wa Casale +1329), lakini pia kufanya umisionari mkubwa hadi India na kuuchochea kama sehemu ya uaminifu wao kwa kanuni.

Mabishano yalichangiwa na Mtumishi mkuu kukosekana muda mrefu au kulemewa na majukumu mengine kutoka kwa Papa.

Viongozi waliofuatana katika ngazi mbalimbali, mara walijaribu kukomesha vikali msimamo mkali, mara waliuunga mkono. Mapapa kadhaa walitumia nguvu, isipokuwa Papa Selestini V (1294), aliyetazamwa kuwa “Papa wa kimalaika” atakayeanzisha Kanisa la Kiroho. Yeye aliwaruhusu waliotaka wajitenge na “jumuia” (walivyojiita umati wa ndugu waliopenda maendeleo) wakaishi upwekeni wakifuata kanuni na wasia bila ya kujali matamko ya Kanisa. Ilikuwa mara ya kwanza kwa shirika kugawanyika.

Alipojiuzulu, mwandamizi wake Papa Bonifasi VIII (1295-1303) alifuta mara maamuzi yake yote, na katika miezi michache iliyofuata aliwaagiza hao Wafransisko Waselestini warudi shirikani, akamuondoa madarakani Mtumishi mkuu aliyewatetea, akamweka mwingine kinyume chao, akawakatalia wasikate rufaa kwake dhidi ya dhuluma.

Viongozi wao, Liberato wa Fossombrone (+1307) na Anjelo Klareno (+1337), walikimbilia Ugiriki wasije wakafungwa tena (waliwahi kukaa gerezani zaidi ya miaka 10).

Hivyo jina la ndugu “wa Kiroho” likawa na maana mpya baadhi yao walipopinga uongozi wa Kanisa, wakitangaza ubatili wa kujiuzulu kwa Selestini V na wa kuchaguliwa Bonifasi VIII; halafu wakadai Mapapa waliotoa matamko juu ya kanuni kuwa wazushi.

Kinyume na mtangulizi wake, Papa Klemensi V (1305-1314) alipenda kusikiliza wote, halafu akatoa (1312) tamko jipya juu ya kanuni ili kuondoa wasiwasi hasa kwa kubainisha amri za kanuni na kiasi ambacho zinawabana Ndugu Wadogo. Ingawa hakukubali msimamo wa ndugu “wa Kiroho” kuhusu mamlaka ya Kanisa juu ya kanuni, aliwaweka chini ya ulinzi wake; viongozi waliowadhulumu waliondolewa, na makosa dhidi ya ufukara yalirekebishwa ili kukwepa farakano. Lakini ikawa bure.

Mara baada ya kuchaguliwa, Papa Yohane XXII (1316-1334), akisukumwa na Mtumishi mkuu Mikaeli wa Cesena (1316-1328), alifululiza kutoa amri zilizolenga kukomesha ndugu “wa Kiroho”, mpaka 4 kati yao walichomwa moto sokoni. Hapo uasi wa wengi ukawa wazi usijali kutengwa na Kanisa wala kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Mwaka 1323 Papa, akiendelea na vita vyake, alitoa hati ya kulaani dhana ya Ndugu Wadogo wote (iliyokubaliwa na mkutano mkuu 1322) kuwa Kristo na mitume hawakumiliki chochote wala binafsi wala kwa pamoja.

Badala ya kukubali tamko hilo, Mtumishi mkuu na wanashirika karibu wote walilikataa hata kumtangaza Yohane XXII kuwa mzushi. Mfalme mkuu wa Ujerumani, ili apate nguvu dhidi ya Papa, akawapokea Ndugu Wadogo chini ya ulinzi wake akafanya mmojawao atangazwe kinyume cha sheria kuwa ni Papa badala ya Yohane XXII (bado hai).

Baadaye kidogo uasi huo ukaisha, lakini matokeo ya kwazo kubwa hivi yalichangia sana kudidimia kwa shirika.

Hasa Waklareno wakaendelea hivyo katika Italia ya Kati zaidi ya miaka mia mpaka Yohane wa Capestrano na Yakobo wa Marka walipowapatanisha na Kanisa (1430 hivi), hata wakarudi chini ya Mtumishi wa shirika lote (1473) wakiwa na Makamu maalumu wa kwao [2].

Uamuzi huo wa Papa Sisto IV ulitekelezwa miaka michache tu, halafu Waklareno walirudi chini ya maaskofu wa majimbo. Ni Papa Pius V, kwa hati Beatus Christus salvatoris ya tarehe 23 Januari 1568, aliyefaulu kuwaunganisha kweli na Waoservanti. [3]

Tanbihi

Marejeo

Loading related searches...

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.