Mapinduzi ya Urusi ya 1917

From Wikipedia, the free encyclopedia

Mapinduzi ya Urusi ya 1917
Remove ads

Mapinduzi ya Urusi ya 1917 ni namna ya kutaja mfuatano wa mapinduzi mawili katika mwendo wa mwaka 1917 yaliyomaliza ufalme wa miaka 1,000 nchini Urusi na kuanzisha utawala wa ukomunisti kwa miaka 70 iliyofuata.

Thumb
Wanajeshi wakiandamana Petrograd

Mwaka 1917 uliona mapinduzi mawili katika Urusi:

na

  • mapinduzi ya Oktoba ambako serikali ya muda ilifukuzwa na utawala wa kikomunisti ulianza.
Remove ads

Utangulizi

Urusi ilikuwa nchi kubwa kuliko zote duniani (hata leo ni hivyo, ila ilipitiwa kwa muda na milki ya Britania au Uingereza iliyotawala eneo kubwa zaidi kwa karne moja hadi mwisho wa ukoloni). Mwaka 1917 Urusi ilikuwa nchi shiriki katika Vita Kuu ya Dunia ya Kwanza pamoja na Uingereza na Ufaransa dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria.

Baada ya mafanikio ya kwanza ya mwaka 1914 jeshi la Urusi lilipaswa kurudi nyuma tangu mwaka 1915. Kushindwa mara kwa mara kuliongeza upinzani dhidi ya utawala wa Tsar Nikolas II wa Urusi.

Matatizo ya kijeshi yaliongeza ukali wa matatizo ya kijamii, kisiasa na ya kiuchumi yaliyotangulia vita ya 1914 na kusababisha tayari mapinduzi ya Urusi ya 1905.

Kati ya matatizo haya yalikuwemo:

  • utaratibu wa kisiasa ulimpa mtawala mkuu yaani tsar madaraka mengi mno na kuzuia matengenezo yaliyohitajika; tsar alikuwa na madaraka ya kutosha ya kupuuza bunge na la kutoa imla kwa serikali
  • utamaduni wa Kirusi ulikuwa na athira kubwa ya serikali kuu iliyojaribu kusimamia uchumi na kukua kwa viwanda
  • nafasi kubwa ya serikali ilikuza tabaka la watumishi wa serikali kwenye ngazi zote waliochelewesha maazimio na kudai hongo
  • kwa jumla maendeleo ya uchumi na teknolojia bado yalikuwa nyuma ya Ulaya ya magharibi
  • sehemu kubwa ya wananchi waliishi vjijini ambako bado taratibu za ukabaila zilisimamia maisha ya wengi na kukwamisha maendeleo
  • jeshi liliongozwa na majenerali makabaila waliodharau askari wa kawaida; kutowaheshimu kulileta mitindo ya vita iliyosababisha vifo vingi

Kwa jumla idadi ya wananchi ambao hawakuridhika na hali ya taifa iliendelea kukua. Vyama vya siasa vyenye mwelekeo wa upinzani vilikuwa na wafuasi kati ya wafanyakazi wa viwanda kwenye miji mikubwa na pia kwenye matabaka ya kati. Wakulima ambao mara nyingi hawakuelewa siasa nje ya kijiji chao waliingia jeshini walipokutana na wafanyakazi na watu wa mjini waliowapa fikra mpya za siasa.

Kushindwa kwa Urusi katika mapigano mbalimbali ya vita kulisababisha hali ya hasira kukua na kuandaa mapinduzi.

Remove ads

Mapinduzi ya Februari 1917

Majira ya baridi kati ya miaka 1916 na 1917 yalileta njaa kwa watu wengi. Mavuno ya 1916 yalikuwa duni kwa sababu ya hali ya hewa na ukosefu wa wafanyakazi kwa sababu wakulima wengi walikuwa wanajeshi vitani. Miezi ya baridi ilileta njaa kwa sababu vyakula havikutosha tena.

Mnamo Januari 1917 wakinamama wa mtaa wa wafanyakazi wa Sankt Petersburg waliamua kuandamana barabarani wakidai chakula. Serikali ilituma wanajeshi dhidi yao waliotumia silaha. Lakini maandamano yaliendelea na askari walianza kukataa amri zao.

Serikali ilivunja bunge ila tu wabunge walisita kutii wakaunda kamati ya kudumu. Katika muda wa masaa 24 wanajeshi wote wa Sankt Petersburg walikataa kutumia silaha dhidi ya wananchi wakajiunga na upinzani. Serikali ya Tsar ikajiuzulu tarehe 13 Machi (iliyokuwa tarehe 28 Februari katika kalenda ya Juliasi).

Hapo bunge liliamua kuchukua madaraka mikononi mwake ikamteua amiri jeshi mpya badala ya tsar Nikola II na kupeleka wawakilishi wake katika wizara. Wakati uleule wafanyakazi wa viwanda vya Sankt Petersburg na pia wanajeshi walianza kuchagua kamati zao na kuunda kamati ya utendaji ya wafanyakazi na wanajeshi. Kamati hizo ziliitwa kwa Kirusisovyeti” na sovyeti zote zilikuwa na sovyeti ya pamoja mjini Sankt Petersburg.

Tsar Nikola II aliyekaa kwenye makao makuu ya jeshi aliamua kuhamia Sankt Petersburg lakini treni yake ikasimamishwa na wanajeshi walioasi akapelekwa mjini Psow penye makao ya sehemu ya kaskazini ya jeshi. Majenerali waliokaa huko hawakuona uwezekano wa kukandamiza mapinduzi, kwa kuwa wanajeshi hawatakubali amri za kutumia silaha dhidi ya wananachi. Walimshauri tsar kujiuzulu akaitikia pia kwa jina la mwanawe. Mdogo wa tsar alitanganza ya kwamba asingekubali utawala naye kwa hiyo tarehe 3 Machi 1917 (15 Machi kwenye kalenda ya kale) utawala wa kifalme ulikwisha nchini Urusi.

Remove ads

Vyombo vya utawala vilivyoshindana tangu Februari 1917

Baada ya kujiuzulu kwa Tsar Nikolai II Urusi ulikuwa na vitovu vitatu vya utawala:

  • Bunge na kamati yake ya kudumu
  • Sovyeti au kamati za wanajeshi na wafanyakazi
  • Jeshi na majenerali wake walioendelea kupigania vita dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria

Majenerali hawakupenda demokrasia lakini walipaswa kuchagua kati ya mtawala wao na taifa kwa jumla wakitaka kuendelea na vita. Waliamua kumwacha mtawala wakijaribu kusalimisha utaratibu kati ya wanajeshi.

Bunge lilikuwa na kamati yake ya kudumu iliyochukua nafasi ya serikali lakini madaraka yake yalipungukiwa. Ndani ya bunge kulikuwa na vikundi mbalimbali. Upande mmoja walikuwa watetezi wa ufalme; nafasi ya katikati walikuwa wawakilishi wa matabaka ya kati waliokuwa tayari kushirikiana na tsar akikubali haki za katiba wakitafuta siasa ya kibepari.

Kwa upande mwingine walikuwepo vyama vya kisoshalisti hasa Chama cha Mapinduzi ya Kijamii pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa Kijamii-Kidemokrasia kilichokuwa kimegawanyaika kabla ya vita katika vikundi vya Mensheviki na Bolsheviki. Bolsheviki walitaka mapinduzi kwa njia ya kijeshi na utawala wa kidikteta utakaobadilisha muundo wa jamii kuelekea ukomunisti. Lakini kundi lenye wafuasi wengi zaidi walikuwa Mensheviki. Bungeni wabunge wa Mapinduzi ya Kijamii na Mensheviki walikuwa wachache kutokana na sheria ya uchaguzi uliowazuia wafanyakazi wengi kwenye kura. Lakini walikuwa na nguvu katika kamati za sovyeti.

Mwanzoni sovyeti hizi za wanajeshi na wafanyakazi zilikuwa na nguvu katika miji mikubwa ya Sankt Petersburg na Moscow pekee. Ila tu Sankt Petersburg walikuwa na uwezo zaidi kwa sababu ilikuwa makao makuu ya serikali. Walifaulu kupata kibali cha serikali mpya ya kuwa kila kikosi cha jeshi kilitakiwa kuchagua sovyeti yake na kutuma wawakilishi kwenye mkutano wa sovyeti ya wanajeshi na wafanyakazi.

Hivyo wakati viongozi wa jeshi walijitahidi kutunza nidhamu kati ya askari na kuwa tayari kwa hali ya vita. Huko Sankt Petersburg serikali ya bunge na kamati za wafanyakazi na wanajeshi ziligawana madaraka bila utaratibu wa wazi. Hasa hawakukubaliana juu ya suala la vita au amani. Ujerumani kama mpinzani mkuu ilikuwa na madai makali sana ambayo yalionekana hayakubaliki kwa Urusi. Lakini wakati huohuo serikali ilikuwa na matatizo kuondoa uhaba wa chakula kwa watu maskini katika miji mikubwa walioendelea kutoridhika.

Remove ads

Kurudi kwa Lenin na siasa ya Bolsheviki

Mwezi wa Aprili 1917 kiongozi wa Bolsheviki Vladimir Ilyich Lenin alirudi Urusi. Lenin aliwahi kukaa Uswisi alipopata kimbilio cha kisiasa. Polisi ya siri ya Ujerumani ilimsafirisha kupitia Ujerumani hadi Skandinavia kwa sababu Wajerumani walitaka kuharakisha mapinduzi katika Urusi. Walilenga kudhoofisha jeshi la Kirusi kwa njia hii.

Lenin alianza mara moja kuwahutubia wafanyakazi wa Sankt Petersburg na kudai amani ya mara moja kwa kukubali madai yote ya wapinzani. Wanasiasa wa vyama vya kisoshalisti nje ya Bolsheviki walipewa tayari wizara kadhaa katika serikali, lakini hawakuwa na athira juu ya maazimio ya kijeshi. Habari za mapigano ambako jeshi la Urusi lilishindwa zilidhoofisha imani ya wananchi katika serikali mpya. Chakula kilikuwa haba na njaa ilizidi.

Hadi Oktoba wawakilishi wengi katika sovyeti za wafanyakazi na wanajeshi mjini Sankt Petersburg walianza kusogea upande wa Lenin na Wabolsheviki.

Remove ads

Mapinduzi ya Oktoba

Katika hali hiyo Lenin na wenzake waliamua kupindua serikali. Trotski alianzisha kamati ya kijeshi ya Sovyeti ya Petrograd. Hapa alitegemea wanajeshi wa ulinzi waliokaa Petrograd pamoja na wanamaji - kati ya viongozi wao Bolsheviki walikuwa wengi. Pia alikuwa na wanamgambo wa chama waliopewa silaha ambao walikuwa wafanyakazi teule kutoka viwandani. Wakuu wa jeshi walikataa kupokea amri kutoka Trotski na tarehe 22 Oktoba alitangaza ya kwamba kamati ya ...

Katika usiku wa 24/25 Oktoba (ya kalenda ya Juliasi; ilikuwa 7/8 Novemba kwenye kalenda ya Gregori) vikosi vya Bolsheviki walitwaa ofisi muhimu za mjini kama ghala za silaha, posta na makao makuu ya huduma ya simu.

Hatimaye kikosi cha Bolsheviki kilitwaa ikulu mjini iliyokuwa makao makuu ya serikali. Mawaziri wote walikamatwa isipokuwa waziri mkuu Kerenski aliweza kukimbia.

Wabolsheviki waliunda serikali mpya chini ya uogozi wa Lenin. Upinzani mjini Sankt Petersburg na pia Moscow ulikuwa mdogo. Lakini nje ya miji mikubwa hali ilikuwa tofauti. Chama cha Bolsheviki iliendelea kutumia wanamgambo na sehemu ya wanajeshi walioshirikiana nao kufukuza wapinzani wote hata vyama vya Kisoshalisti vingine kama Mensheviki na Wanamapinduzi wa Kijamii.

Remove ads

Kufukuzwa kwa bunge la katiba

Tar 12/25 Novemba 1917 ulitokea uchaguzi kwa bunge la kutunga katiba mpya. Uchaguzi huo uliwahi kuamuliwa na bunge la zamani na kuandaliwa na serikali ya Kerenski. Lenin alitangaza ya kwamba bunge jipya litakuwa na madaraka ya kuamua juu ya wakati ujao. Lakini uchaguzi wenyewe ulielekea tofauti; Bolsheviki walipata asilimia 20-25 za kura tu. Walishinda katika miji mikubwa na kati ya wanajeshi, lakini idadi kubwa ya wananchi vijijini waliokuwa wengi walipigia kura chama cha Mapinduzi ya Kijamii kilichopata zaidi ya nusu ya wabunge wote.

Chama Kura Wabunge
Chama cha Mapinduzi ya Kijamii 17,100,000 380
Bolsheviki 9,800,000 168
Mensheviki 1,360,000 18
Chama cha Demokrasia 2,000,000 17
Wawakilishi wa makabila 77
Chama cha Mapinduzi cha Kijamii – kitengo cha kushoto 39
Wasoshalisti wa taifa 4
Jumla: 41,700,000 703[1]

Bunge hilo lilikutana mara moja tu kwa masaa machache. Wabolsheviki walipoona ya kwamba wengine hawafuati waliondoka wakafukuza wabunge kwa wanajeshi wao.

Remove ads

Amani na Ujerumani

Serikali mpya ilitangaza mara moja iko tayari kumaliza vita ikaingia haraka katika majadiliano na Wajerumani ikakubali masharti yote ya Wajerumani. Mapigano yote yalisimamishwa tarehe 15 Desemba 1917 na mkataba wa amani kati ya Urusi na Ujerumani ulitiwa sahihi katika Machi ya 1918.

Amani hiyo iliruhusu wanajeshi kurudi nyumbani; jeshi lenyewe liliporomoka na athira ya Bolsheviki ilipanuka hata nje ya miji mikubwa wakaonekana kwa watu wengi kama wakombozi waliomaliza mauaji.

Remove ads

Vita ya wenyewe kwa wenyewe

Tokeo la mapinduzi ya Kibolsheviki lilikuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Urusi. Zaidi ya watu milioni 8 walikufa hadi 1921 ushindi wa Wabolsheviki ulipopatikana.

Tanbihi

Marejeo

Viungo vya nje

Loading related searches...

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Remove ads