Jamhuri ya Watu wa China
From Wikipedia, the free encyclopedia
China, rasmi inajulikana kama Jamhuri ya Watu wa China (PRC), ni nchi kubwa iliyoko Asia ya Mashariki. Ni taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, zaidi ya bilioni 1.4, ikishika nafasi ya pili kwa idadi ya watu. China inapakana na nchi 14: kaskazini na Mongolia na Urusi, magharibi na Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Afghanistan, na Pakistani, kusini na India, Nepal, Bhutan, Myanmar, Laos, na Vietnam na mashariki na Korea Kaskazini. Mji wake mkuu ni Beijing na Shanghai ikiwa kitovu cha uchumi. Ikiwa na eneo la takriban kilomita za mraba milioni 9.6, China ni nchi ya nne kwa ukubwa duniani, ikiwa na mandhari mbalimbali kama milima, nyanda za juu, na pwani.
"China" inaelekezwa hapa. Kwa Taiwan, tazama Jamhuri ya China.
Jamhuri ya Watu wa China Zhōnghuá Rénmín Gònghéguó (Kimandarini) | |
---|---|
Wimbo wa taifa: "March of the Volunteers" | |
Mji mkuu | Beijing |
Mji mkubwa | Shanghai |
Lugha rasmi | Kimandarini cha Kawaida |
Lugha ya taifa | Kimandarini |
Kabila | 91.1% Wahan 8.9% Wengine |
Dini | |
Serikali | Jamhuri ya kijamaa ya chama kimoja cha Kimarxisti-Leninisti |
• Katibu Mkuu wa CCP na Rais | Xi Jinping |
• Waziri Mkuu | Li Qiang |
Historia | |
• Nasaba ya kwanza kabla ya ufalme | 2070 BCE |
• Nasaba ya kwanza ya kifalme | 221 BCE |
• Katiba ya sasa | 1 Januari 1948 |
• Tangazo la Jamhuri ya Watu | 1 Oktoba 1949 |
Eneo | |
• Jumla | km2 9,596,961 km² (ya 4) |
• Maji (asilimia) | 2.8% |
Idadi ya watu | |
• Kadirio la 2024 | 1,408,280,000 |
• Msongamano | 147/km2 |
PLT (PPP) | Kadirio la 2024 |
• Jumla | ▲ $37.072 Trilioni [1] |
• Kwa kila mtu | ▲ $26,310 [1] |
PLT (Kawaida) | Kadirio la 2024 |
• Jumla | ▲ $18.273 Trilioni [1] |
• Kwa kila mtu | ▲ $12,969 [1] |
HDI (2022) | ▲ 0.788 juu sana |
Gini (2021) | 35.7 |
Sarafu | Renmimbi ¥ (CNY) |
Majira ya saa | UTC+8 (CST) |
Upande wa magari | Kulia Kushoto (Hong kong) |
Msimbo wa simu | +86 (bara) +852 (Hong Kong) +853 (Macau) |
Jina la kikoa | .cn (bara) .hk (Hong Kong) .mo (Macau) |
China inatawaliwa na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP), ambacho kimeendeleza mfumo wa chama kimoja cha kisiasa tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949. Chini ya mfumo huu, nchi imepitia mabadiliko makubwa, hasa kupitia mageuzi ya kiuchumi yaliyoanzishwa mwishoni mwa karne ya 20. Mageuzi haya yalibadilisha uchumi kutoka mfumo wa mipango ya kati kwenda kwenye mfumo unaoongozwa na soko, na kusababisha ukuaji wa haraka wa viwanda, mijini, na ongezeko kubwa la ushawishi wa kiuchumi duniani. Leo, China ni ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani kwa kipimo cha PLT(Pato la taifa) ya kawaida, na ya kwanza kwa kipimo cha Usawa wa nguvu ya ununuzi (PPP).
Mbali na kupanda kwake kiuchumi, China ina nafasi ya kipekee katika masuala ya kimataifa. Ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na inashiriki kikamilifu katika mashirika ya kimataifa kama Shirika la Biashara Duniani (WTO), kundi la BRICS, na Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO). Mpango wa Ukanda na Njia (Belt and Road Initiative) ulioanzishwa mwaka 2013 unalenga kuboresha muunganiko wa kanda na ushirikiano wa kiuchumi barani Asia, Afrika, na Ulaya. Licha ya ushawishi wake unaokua, China inakabiliana na changamoto ngumu, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya idadi ya watu, na mvutano wa kikanda, hasa kuhusu Taiwan, Bahari ya China Kusini, na uhusiano wake na mataifa makuu duniani.
Jiografia
China ina eneo la kilomita za mraba milioni 9.6 hivyo ni nchi ya tatu au ya nne[2] kwa ukubwa duniani.
Sura ya nchi inaonyesha tabia tofautitofauti.
Upande wa kaskazini, mpakani mwa Siberia na Mongolia, kuna maeneo yabisi pamoja na jangwa la Gobi.
Kinyume chake upande wa kusini, mpakani mwa Vietnam, Laos na Burma, hali ya hewa ni nusutropiki yenye mvua nyingi inayolisha misitu minene.
Sehemu za magharibi zina milima mingi ambayo ni kati ya milima mirefu duniani kama Himalaya na Tian Shan.
Mashariki ya nchi huwa na tambarare zenye rutuba na hapa ndipo kanda lenye wakazi wengi.
Upana wa China kati ya kaskazini na kusini ni kilomita 4,200 na kati ya mashariki na magharibi ni kilomita 4,200.
Pwani ina urefu wa kilomita 14,400.
Kuna mito mikubwa; mrefu zaidi ni Yangtse (km 6,300), Hwangho au Mto Njano, Xi Jiang au mto wa Magharibi, Mekong, Mto wa Lulu, Brahmaputra na Amur. Mito hiyo yote ina vyanzo vyake katika milima mikubwa yenye usimbishaji mwingi, ikibeba maji kwenda tambarare pasipo mvua nyingi.
Jiografia hiyo ilikuwa chanzo cha kilimo cha umwagiliaji na kukua kwa madola ya kwanza.
Kutokana na madawa ya kilimo na maji machafu ya viwanda, mito na maziwa ya China hupambana na machafuko makali; mwaka 2007 ziwa Tai lilisafishwa kwa gharama kubwa mno kwa sababu maji hayakufaa tena kwa mahitaji ya binadamu (maji ya bomba).
Hali ya hewa

Kuna kanda 18 za hali ya hewa zinazoonyesha tofauti kubwa kati yake. Upande wa magharibi, kaskazini na kaskazini-mashariki huwa na majira yenye joto kali na baridi kali. Upande wa kusini ina tabia ya tropiki au nusutropiki. Tibet huwa na hali ya hewa kulingana na kimo chake juu ya mita 4,000.
Ramani ya usimbishaji inaonyesha ya kwamba kilimo kinawezekana katika nusu ya kusini na kusini-mashariki ya nchi tu. Upande wa kaskazini na magharibi mvua ni chache mno. Mstari mwekundu unaonyesha mpaka na juu yake usimbishaji ni chini ya milimita 390 kwa mwaka.
Historia

Historia ya China hugawanyika katika vipindi vya nasaba za kifalme mbalimbali. Vipindi muhimu zaidi ni kama ifuatavyo:
- Nasaba ya Qin (221 – 207 KK)
- Nasaba ya Han (206 KK – 220 BK)
- Kipindi cha milki tatu (220 – 280)
- Nasaba ya Jin (265 – 420)
- Kipindi cha nasaba za kusini na kaskazini (420 – 581)
- Nasaba ya Sui (581 – 618)
- Nasaba ya Tang (618 – 907)
- Nasaba tano na milki kumi (907 – 960)
- Nasaba ya Song (960 – 1279)
- Nasaba ya Yuan (1279 - 1368)
- Nasaba ya Ming (1368 - 1644)
- Nasaba ya Qing (1644 - 1911)
Utawala wa kifalme uliendelea hadi mapinduzi ya China ya 1911.
Baada ya kipindi cha vurugu, jamhuri ya China ilitawaliwa na chama cha Kuomintang chini ya rais Chiang Kai-shek.
Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia sehemu kubwa ilitwaliwa na Japani. Wakati huo Chama cha Kikomunisti cha China kiliandaa jeshi kikapambana na serikali ya Kuomintang na Japani pia.
Baada ya mwisho wa vita kuu Wakomunisti waliendelea kupingana na serikali na mwaka 1949 Kuomintang ilishindwa. Wakomunisti chini ya Mao Zedong walianza kutawala China Bara kama Jamhuri ya Watu wa China na Kuomintang walikimbilia kisiwa cha Taiwan walipoendelea kutawala kama "Jamhuri ya China".
Siasa

Serikali ya China inatawala kwa mfumo wa udikteta chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti ya China. Kuna vyama vidogo pia, lakini hivi havina umuhimu wowoteː vinasimamiwa na Wakomunisti, hivyo hali halisi ni mfumo wa chama kimoja.
Kikatiba chombo kikuu ni Bunge la umma la China linalomchagua rais, serikali, mahakama kuu, kamati kuu ya kijeshi na mwanasheria mkuu. Lakini hali halisi maazimio yote ya bunge ni utekelezaji tu wa maazimio ya uongozi wa chama cha Kikomunisti.
Uongozi huo ni kundi dogo la wakubwa wa chama na jeshi. Mwanasiasa muhimu ni Xi Jinping. Kwa sasa yeye anaunganisha vyeo vya Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China na mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi. Kwa jumla katika mapokeo ya Kikomunisti vyeo vya chama ni muhimu kuliko vyeo vya serikali ingawa katiba na sheria inasema tofauti.
Kuna pia "maeneo yenye utawala wa pekee" ambayo ni Hongkong na Macau. Katika miji hiyo miwili, iliyokuwa makoloni ya Uingereza na Ureno, kuna uhuru wa kisiasa na wa uandishi, uchaguzi huru na upinzani kwa kiasi fulani, lakini maeneo yana tu madaraka kadhaa ya kujitawala kwa mambo ya ndani.
Demografia

China ikiwa na wakazi milioni 1,400 (Januari 2020) ni nchi yenye watu wengi zaidi duniani. Historia yake yote iliona tena na tena vipindi vya njaa kutokana na idadi kubwa ya watu wake. Msongamano wa watu kwa wastani ni wakazi 145 kwa kilomita ya mraba. Lakini tofauti ziko kubwa kati ya miji mikubwa ambako milioni 115 wanakaa kwenye eneo la km² 50,000 na Tibet yenye watu 2 tu kwa kilomita ya mraba.
Zaidi ya asilimia 90 za wakazi wote wanakaa katika theluthi ya kusini-mashariki ya nchi yenye mvua ya kutosha. Ndani ya theluthi hiyo ni nusu ya Wachina wote wanaosongamana kwenye asilimia 10 za China yote, maana yake katika 10% hizi kuna msongamano wa watu 740 kwa km².
Wakazi walio wengi ni Wahan au Wachina wenyewe. Wanatumia hasa lahaja mbalimbali za lugha ya Kichina. Pamoja na Wahan kuna makabila 55 yaliyotambuliwa na serikali. Kwa jumla lugha hai ni 292 ambazo zinahusika na makundi mbalimbali ya lugha (angalia orodha ya lugha za China).
Dini
Serikali inafuata rasmi ukanamungu, lakini inaruhusu dini kwa kiasi fulani. Pamoja na hayo, dhuluma zinaendelea dhidi ya madhehebu mbalimbali. Takwimu hazieleweki, pia kwa sababu kabla ya Ukomunisti kupinga dini, hasa wakati wa Mapinduzi ya utamaduni, watu waliweza kuchanganya mafundisho na desturi za Ukonfusio, Utao na Ubuddha. Leo wanaoendelea kufanya hivyo wanakadiriwa kuwa asilimia 30-80 za wakazi. Wabuddha ni 6-16%, Wakristo (hasa Waprotestanti, halafu Wakatoliki na kidogo Waorthodoksi) ni 2-4%, Waislamu ni 1-2%.
Tazama pia
Tanbihi
Marejeo
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.