Marekani
nchi katika Amerika Kaskazini From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Marekani, rasmi Muungano wa Madola ya Amerika (Kiingereza: United States of America, kifupi: USA) ni nchi iliyomo Amerika Kaskazini, na inapakana na Kanada upande wa kaskazini na Meksiko upande wa kusini. Inajumuisha majimbo 50, wilaya ya shirikisho, na maeneo ya nje. California na Texas ndiyo majimbo yaliyokuwa na watu wengi zaidi. Marekani ina takriban watu milioni 340 na kuwa nchi ya tatu duniani kuwa na watu wengi sana. Aidha, ni nchi ya tatu kwa ukubwa duniani, ikiwa na eneo la takriban kilomita za mraba milioni 9.8, ikienea kutoka Bahari ya Atlantiki hadi Bahari ya Pasifiki.Mji mkuu wa Marekani ni Washington DC. Los Angeles, New York na Chicago ndio miji mikubwa
Marekani ina jiografia na hali ya hewa tofauti, ikianzia kwenye tundra ya Aktiki huko Alaska hadi fukwe za kitropiki huko Florida na Hawaii. Mandhari yake inajumuisha safu kuu za milima kama Rockies na Appalachians, nyanda pana, na mito mikubwa kama Mississippi na Missouri (mto). Nchi hii ina utajiri mkubwa wa rasilimali za asili na ina sekta kubwa za kilimo, viwanda, na teknolojia ambazo zinachangia hadhi yake kama uchumi mkubwa zaidi duniani kwa kipimo cha Pato la Taifa (GDP) la kawaida, na kituo kikuu cha uvumbuzi, utamaduni, na nguvu za kijeshi.
Marekani ilianzishwa mwaka 1776 kupitia Tangazo la Uhuru la Marekani, kufuatia mapambano ya makoloni kumi na tatu dhidi ya utawala wa Uingereza. Tangu wakati huo, imepanuka kote Amerika ya Kaskazini na kujitokeza kama nguvu ya dunia, hasa baada ya vita vya dunia vya karne ya 20. Marekani ni jamhuri ya shirikisho inayozingatia katiba na demokrasia ya uwakilishi, yenye serikali inayotawaliwa na mfumo wa mizania ya madaraka kati ya matawi ya utendaji, kutunga sheria, na mahakama. Ni mwanachama mwanzilishi wa mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, NATO, na Benki ya Dunia, na inaendelea kucheza nafasi ya uongozi katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni duniani.
Remove ads
Demografia
Kufikia katikati ya mwaka 2024, idadi ya Wakazi wa Marekani imefikia takriban milioni 340, ikionyesha ongezeko la asilimia 2.6 tangu Sensa ya 2020. Mandhari ya kidemografia ya taifa hili inazidi kuwa mchanganyiko: Wazungu wasio wa asili ya Kihispania ni takriban asilimia 57.8, Wahispania au Walatino 18.7%, Wamarekani Weusi 12.1%, na Wamarekani wa asili ya Asia 5.9%. Kiwango cha uzazi kimeshuka hadi wastani wa watoto 1.6 kwa kila mwanamke, chini ya kiwango cha kuzaliana kinachohitajika, huku umri wa wastani ukiwa umeongezeka hadi takriban miaka 39.1, jambo linaloonyesha wazi mwelekeo wa kuzeeka kwa idadi ya watu. Uhamiaji unabakia kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji: mnamo 2024, karibu asilimia 84 ya ongezeko la idadi ya watu lilitokana na wahamiaji, huku jamii za Wahispania na Waasia zikionyesha ukuaji mkubwa (asilimia 9.7% na 13%, mtawalia).
Idadi ya wakazi
Kabila/Asili

Kijerumani Marekani Meksiko Kieire Kiafrika Kiitalia Kiingereza Kijapani Puerto Rico
Kufikia mwaka 2025, Wazungu wasio wa asili ya Kihispania bado ndio kundi kubwa zaidi nchini Marekani, wakichukua takriban asilimia 57.6 ya idadi ya watu. Wahispania au Walatino ndio kundi la wachache linalokua kwa kasi zaidi, likiwakilisha takribani asilimia 19–20. Wamarekani Weusi au Waafrika Wamarekani wanaunda takribani asilimia 12–14 ya idadi ya watu. Wamarekani wa asili ya Asia ni takribani asilimia 6–7, wakiwa takriban watu milioni 22 (6.49%) kufikia katikati ya 2024. Machotara pia ni kundi linaloongezeka kwa kasi, sasa wakiwa takriban asilimia 3–5 ya idadi ya watu. Makundi madogo zaidi ni pamoja na Wamarekani wa asili na Wakaazi wa Alaska (takribani asilimia 1–2) na Wenyeji wa Hawaii au Visiwa vya Pasifiki (chini ya asilimia 1). [6]
Lugha
Marekani ina mazingira yenye mchanganyiko mkubwa wa lugha, ambapo zaidi ya lugha 350 huzungumzwa kote nchini. Takwimu za mwaka 2020 zinaonyesha kuwa asilimia 78 ya wakazi huzungumza Kiingereza pekee nyumbani, huku asilimia 22 wakitumia lugha nyingine. Kati ya kundi hili, Kihispania kinachukua asilimia 13, kikifuatwa na Kichina (1.1%), Kitagalog (0.6%), Kivietinamu (0.5%), Kiarabu (0.5%), Kifaransa (0.4%), Kikorea (0.3%) na Kirusi (0.3%). Lugha za kiasili zinabaki na sehemu ndogo chini ya 0.5%, huku Kinavajo kikiwa na wasemaji wengi zaidi. [7]
Dini
Dini nchini Marekani inaonyesha mchanganyiko mkubwa wa imani na mwenendo wa kubadilika kwa muda. Kulingana na takwimu za hivi karibuni, asilimia 62 ya watu wazima wanajitambulisha kuwa Wakristo huku wengi wao wakiwa Waprotestanti (40%), Wakatoliki (19%), na makundi mengine ya Kikristo (3%). Asilimia 29 hawana uhusiano wa kidini, kundi linalojumuisha wasiomwamini Mungu (5%), wanaotilia shaka (6%), na wasiokuwa na maelezo maalum (19%). Dini nyingine zisizo za Kikristo zinachukua asilimia 7, zikiwemo Wayahudi (2%), Waislamu (1%), Wabudha (1%), Wahindu (1%), na zingine ndogo zaidi. Hata hivyo, imani za kiroho zinabaki kuwa na ushawishi mpana, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaamini katika Mungu, roho au nguvu ya juu.[8]
Muundo wa Umri
Umri wa kati: miaka 38.5 (2021).
Elimu

Elimu nchini Marekani ina kiwango cha juu cha ushirikishwaji, ambapo takribani asilimia 91 ya watu wenye umri wa miaka 25 na zaidi wamekamilisha angalau elimu ya sekondari, na karibu asilimia 38 wamehitimu elimu ya chuo kikuu au zaidi. Kati ya wakazi hao, asilimia 28 wana elimu ya sekondari pekee, 15 elimu ya chuo bila shahada, 10 shahada ya kati (associate degree), 23 shahada ya kwanza, na 14 elimu ya juu zaidi kama shahada ya uzamili, kitaaluma au uzamivu.
Kipato na Umaskini
Watu maarufu
- Abraham Lincoln
- Al Capone
- Barack Obama
- Beyoncé Knowles
- Bill Gates
- Bob Dylan
- Donald Trump
- Elvis Presley
- Franklin D. Roosevelt
- George Gershwin
- George Washington
- Henry Ford
- Hillary Rodham Clinton
- John Kennedy
- Louis Armstrong
- Madonna
- Malcolm X
- Martin Luther King
- Michael Jackson
- Michael Jordan
- Miles Davis
- Oprah Winfrey
- Rosa Parks
- Steve Jobs
- Thomas Edison
- Thomas Jefferson
- Walt Disney
- William Edward Burghardt Du Bois
Remove ads
Jiografia
Marekani bara

Eneo la Marekani lina ukubwa wa kilometa mraba 9,826,675 na liko hasa katika bara la Amerika Kaskazini kati ya Kanada upande wa kaskazini na Meksiko upande wa kusini.
Marekani imeunganisha upana wote wa bara kutoka Bahari ya Atlantiki hadi Pasifiki, ikigawanywa kwa majimbo 48 yanayojitawala.
Eneo hilo lagawiwa katikati na mto mkubwa Mississippi unaoanza mpakani kwa Kanada na kuishia katika Ghuba ya Meksiko.
Alaska
Jimbo la Alaska liko pia kwenye bara la Amerika Kaskazini upande wa kaskazini kutoka Kanada kuelekea Urusi, lakini halipakani na jimbo lolote la Marekani.
Hawaii
Funguvisiwa la Hawaii ni jimbo la visiwani katika bahari ya Pasifiki. Ni jimbo la 50 na la mwisho mpaka sasa.
Visiwa vya ng'ambo vya Marekani
Maeneo ya ng'ambo ya Marekani ni visiwa kadhaa ambavyo ni maeneo ya Kimarekani ingawa si sehemu ya jimbo lolote. Zamani yalikuwa kama makoloni hata kama Marekani ilidai kutokuwa na ukoloni. Siku hizi maeneo haya yamepata viwango mbalimbali vya kujitawala. Kwa kawaida maeneo haya huchagua pia wawakilishi kwa ajili ya bunge la Marekani lakini wawakilishi hao si wabunge wa kawaida, bali wana haki ya kusema na kushauri tu bila haki ya kupiga kura.
Visiwa muhimu kati ya hivyo ni kama ifuatavyo:
- Puerto Rico (Karibi)
- Visiwa vya Virgin vya Marekani (Karibi)
- Visiwa vya Mariana (Pasifiki)
- Guam (Pasifiki)
Milima
angalia: Orodha ya milima ya Marekani
Safu ya milima ya Rocky Mountains inavuka Marekani yote kutoka kaskazini hadi kusini upande wa magharibi.
Mito
angalia: Orodha ya mito ya Marekani
Mto mkubwa wa Marekani ni Mto Mississippi.
Remove ads
Historia

Historia ya awali inaanza na kilele cha Enzi ya barafu, watu wa Asia walipoweka kuingia Alaska kupitia nchi kavu. Baada ya hapo watu hao na wajukuu wao hawakuwa tena na uhusiano na wale wa "Dunia ya zamani" (Afrika, Asia na Ulaya) mpaka walipofikiwa na Wazungu kutoka Norway (karne ya 10) na Christopher Columbus mwaka 1492.
Hao wakazi wa kwanza walikuwa wawindaji-wakusanyaji; wakifuata mawindo yao walifika taratibu hadi ncha ya kusini ya Amerika (Tierra del Fuego).
Polepole utamaduni wa baadhi ya makabila, ingawa kwa kuchelewa kuliko Dunia ya zamani, ulifikia hadhi ya ustaarabu, kama vile ule wa Mississippi.
Safari za baharia Christopher Columbus kuanzia mwaka 1492, zilivuta hasa Hispania, Ureno na halafu Uingereza, Ufaransa na Uholanzi kujianzishia makoloni ili kunyonya maliasili nyingi za "Dunia mpya".
Kwa namna hiyo, mazingira ya Amerika yalibadilika kabisa mpaka zikatokea aina mpya za utamaduni na hatimaye mataifa mapya, hasa kutokana na mchanganyiko ya wenyeji (Waindio) na walowezi kutoka Ulaya, halafu pia watumwa kutoka Afrika.
Marekani ilianza kama muunganiko wa makoloni ya Uingereza kwenye pwani ya mashariki ya Amerika ya Kaskazini tangu karne ya 17. Walowezi kutoka Uingereza walijipatia ardhi wakipigana na wenyeji Waindio.
Tangu karne ya 19 wahamiaji walifika pia kutoka Asia, hasa China na Japani.
Katika vita dhidi ya Hispania na Meksiko, Marekani ilipanua eneo lake kwenda kusini.
Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Marekani ilipigwa kuanzia 1861 hadi 1865 kati ya majimbo ya kusini na majimbo ya kaskazini nchini Marekani. Sababu mojawapo muhimu ya vita ilikuwa suala la utumwa. Majimbo ya kaskazini yaliwahi kupiga utumwa marufuku lakini majimbo ya kusini yaliendelea na sheria zilizoruhusu utumwa na matajiri wengi wa kusini walitegemea kazi ya watumwa hao. Mafarakano yalianza kuhusu swali kama madola mapya yaliyoanzishwa katika Amerika Kaskazini na kujiunga na Muungano yangeruhusiwa kukubali utumwa au la. Mwaka 1861 madola ya kusini-mashariki yalitangaza kujiondoa katika Muungano na kuanzisha "Shirikisho la Madola ya Amerika". Vita vilianza na kudumu miaka minne na watu 650.000 walikufa, lakini mwishoni kaskazini ilishinda. Utumwa ulipigwa marufuku na watumwa walipewa haki za kiraia. Lakini watumwa wengi wa awali waliendelea kuwa maskini na baada ya muda, sheria mpya katika majimbo ya kusini zilinyima haki nyingi za kiraia za Wamarekani weusi waliopaswa kuishi chini mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Katika miongo iliyofuata, Marekani ilitwaa maeneo yaliyowahi kubaki chini ya mamlaka ya Waindio na kuyafanya maeneo yake. Katika Vita vya Marekani dhidi ya Hispania kwenye mwaka 1898 ilijipatia utawala juu ya Ufilipino na Puerto Rico, makoloni ya awali ya Hispania, na kuwa yenyewe nchi iliyotawala makoloni.
Wahamiaji kwa mamilioni waliendelea kufika hasa kutoka Ulaya. Kabla ya mwaka 1880 idadi kubwa walitoka Ujerumani, Eire, Uingereza na Uskoti, pamoja na Wachina waliotafuta kazi hasa Kalifornia. Baada ya mwaka 1880 hadi Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914-1918) wengi walifika kutoka Ulaya ya Kusini na ya Mashariki, hasa Waitalia, Wayahudi kutoka Milki ya Urusi, Wapolandi na wenyeji wa nchi nyingine za Kislavi. Wahamiaji hao walileta pia tamaduni zao na kukubali mishahara midogo kuliko wenyeji waliowahi kufika mapema; hali hiyo ilileta mara kadhaa sheria zilizolenga kuweka mipaka; sheria ya mwaka 1882 ilikataa kufika kwa Wachina, sheria ya mwaka 1922 ililenga kupunguza idadi ya Waitalia, Wayahudi na watu wa Ulaya ya Mashariki kwa kutaja mipaka kwa kila nchi ya asili[10].
Katika siasa ya nje, Marekani iliwahi kutangaza tangu mwaka 1823 kwamba ilitazama Amerika yote kama eneo ambalo haikubali kuingiliwa na nchi za Ulaya; wakati ule makoloni mengi ya Amerika ya Kusini yalikuwa yakifaulu kupata uhuru kutoka Hispania, na Marekani ilitaka kusisitiza isingekubali kuingia kwa mataifa mengine ya Ulaya.
Katika miongo iliyofuata uchumi wa Marekani uliimarika pamoja na kukua kwa sekta ya viwanda na wafanyabiashara wa Marekani walipanua biashara yao kimataifa; mnamo 1854 manowari za Marekani ziliilazimisha Japani kukubali kufunguliwa kwa ubalozi na kupokea wafanyabiashara. Meli za wafanyabiashara wa Marekani zilifika kote duniani, tangu miaka ya 1830 hadi Zanzibar ambako ubalozi mdogo ulifunguliwa mwaka 1837[11]. Wakati wa vita dhidi ya Hispania Marekani ilihakikisha pia nafasi yake katika biashara ya China dhidi ya mipango ya mataifa ya Ulaya ya kuigawa nchi hiyo.
Mwaka 1917 Marekani iliingia katika Vita Vikuu vya Kwanza upande wa Uingereza na Ufaransa; baada ya vita rais Woodrow Wilson alishawishi mataifa mengine kuanzisha Shirikisho la Mataifa lakini bunge lilizuia kuingia kwa Marekani katika umoja huo.
Mdororo Mkuu wa mwaka 1929 ulileta matatizo makubwa kwa uchumi na hata njaa kwa raia wengi lakini ulileta pia siasa mpya ya "New Deal" chini ya rais Franklin D. Roosevelt ambako kwa mara ya kwanza programu za kisiasa zilitumia mapato ya serikali kwa shabaha ya kusaidia idadi kubwa ya wananchi waliokuwa bila kazi, bila nyumba na bila kipato; vijana kwa mamilioni waliajiriwa na serikali kwa kazi ya kujenga miundombinu (barabara, mifereji) na kuboresha hifadhi za taifa.
Mwaka 1941 Marekani iliingia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia baada ya kushambuliwa na Japani na kupokea tangazo la vita kutoka Ujerumani. Uwezo wa kiuchumi wa Marekani ulileta ushindi wa mataifa ya ushirikiano. Uwezo wake wa kisayansi ulipanuliwa na wanasayansi kama Albert Einstein waliopaswa kukimbia udikteta wa Adolf Hitler katika Ujerumani na kuiwezesha kutengeneza mabomu ya kwanza ya nyuklia yaliyotumika mnamo Agosti 1945 kuteketeza Hiroshima na Nagasaki.
Katika miongo ya vita baridi iliyofuata, Marekani ilikuwa taifa la kuongoza nchi zenye demokrasia na pia zile ambazo zilisimama upande wa ubepari tu bila demokrasia dhidi ya nchi za kikomunisti zilizoongozwa na Umoja wa Kisovyeti.
Mwanzo wa miaka ya 1960 ilishindana na Umoja wa Kisovyeti katika mbio wa kuingia katika anga-nje ikafaulu kupeleka watu wa kwanza hadi Mwezi mnamo Agosti 1969. Kutokana na ushindani na nchi za ukomunisti Marekani iliingia katika Vita ya Vietnam hadi kushindwa mwaka 1975.
Vilevile miaka ya 1960 ilikuwa kipindi cha mapambano kwa ajili ya haki za Wamarekani weusi, wajukuu wa watumwa wa awali hasa kusini mwa Marekani. Sheria zilizotenganisha watu pamoja na matumizi ya shule, vyuo, majengo na taasisi za burudani kulingana na rangi ya ngozi, zilizozuia ndoa kati ya watu wa rangi tofauti na kuzuia watu maskini wasitumie haki za kiraia zilipigwa marufuku bila kuondoa tofauti katika uwezo wa kiuchumi kati ya makundi katika jamii.
Mapinduzi ya kiteknolojia ya kompyuta na intaneti yalienea Marekani haraka kushinda sehemu nyingine za Dunia.
Remove ads
Tazama pia
Marejeo
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads