Jumuiya ya Afrika Mashariki
Shirika la Kisiasa katika Afrika mashariki From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni shirika la kisiasa kati ya nchi nane za kanda ya Maziwa Makuu ya Afrika: Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania, na Uganda. Lengo kuu la EAC ni kukuza ushirikiano wa kikanda katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, forodha, na ushirikiano wa kisiasa. Jumuiya hii ilianzishwa awali mwaka 1967, lakini ilisambaratika mwaka 1977 kutokana na tofauti za kisiasa, kabla ya kufufuliwa rasmi mwaka 2000 kwa kutiwa saini kwa mkataba mpya. Kufikia mwaka 2024, William Ruto, Rais wa Kenya, ndiye mwenyekiti wa sasa wa EAC.
Kwa nchi iliyopendekezwa, tazama Shirikisho la Afrika Mashariki.
Tangu kufufuliwa kwake, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanzisha hatua mbalimbali muhimu za ujumuishaji, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha mwaka 2005, Soko la Pamoja mwaka 2010, na juhudi zinazoendelea kuelekea Muungano wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa. EAC pia imekuwa ikifanya kazi ya kuoanisha sera katika sekta kama usafiri, afya, elimu, na nishati. Ikiwa na jumla ya watu wanaozidi milioni 300 na msisitizo wa pamoja juu ya maendeleo ya kikanda, EAC ina nafasi inayoongezeka katika masuala ya bara na inachukuliwa kama mfano wa ushirikiano wa kikanda barani Afrika.[1][2][3][4]
Kwa sasa eneo la Mtangamano ni km2 4,810,363, likiwa na wakazi 312,362,653 (kadirio la mwaka 2022), hivi kwamba ingekuwa nchi moja tu ingekuwa ya nne duniani.
Remove ads
Demografia
Idadi ya Watu
Jumuiya ya Afrika Mashariki ina idadi ya watu takriban milioni 333.93 ambapo aslimia 31 wanaishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo , Sudan Kusini ndiyo iliyo na watu wachache sana ikiwa na watu takriban milioni 11.48 .Asilimia ya wakazi wanaoishi mijini ni 20 tu, lakini wanaongekeza kwa 4.71% kila mwaka
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kulingana na Idadi ya watu
- Kongo JK 105.83 (31.7%)
- Tanzania 66.62 (19.9%)
- Kenya 55.53 (16.6%)
- Uganda 48.86 (14.6%)
- Somalia 18.36 (5.49%)
- Rwanda 13.95 (4.17%)
- 13.69 (4.09%)
- Sudan Kusini 11.48 (3.43%)
Dini
Ukristo ndiyo dini kubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa na wafuasi milioni 261.86 na asilimia 79% ya watu wa EAC, Kongo,JK ndio iliyo na wafuasi wengi takriban milioni 100 au asilimia 95.4 . Uislamu ina wafuasi takriban milioni 56.69 ambayo ni asilimia 16.98 ya watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiongozwa na Somalia ambapo 99 ni waislamu. Dini za jadi ni asilimia 2.4% haswaa Sudan Kusini ambapo asilimia 35 ni wafuasi wa dini za jadi, Wasio na dini ni asilimia 1.75%
Mgawanyo wa Dini katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
- Ukristo 261.86 (78.4%)
- Uislamu 56.69 (17.0%)
- Dini za Jadi 8 (2.40%)
- Wasio na Dini 5.83 (1.75%)
- Zingine 1.53 (0.46%)
Lugha
Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa ndizo Lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kiswahili hutumika kama Lingua Franca katika nchi hizi huku Kiingereza na Kifaransa zikitumika kama lugha za kufundishia shuleni. Lugha za Jumuiya ya Afrika mashariki zimegawanyika katika kundi tatu ambazo ni Lugha za Kibantu ambayo ndiyo kundi kubwa ya Lugha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Lugha za Kinilotiki na Lugha za Kikushi.
Mijini na Vijijini
Asilimia ya watu walioishi mijini katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni 35% na walioishi Vijijini asilimia 64%. Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndizo nchi zilizokuwa na asilimia kubwa ya wakazi wa mijini zikiwa na asilimia 46% na 45% mtawaliwa. Burundi na Sudan Kusini ndizo nchi zilizokuwa na wakazi wa mjini wachache sana zikiwa na asilimia 13% na 17% ya wakazi wanaoishi mijini huku asilimia 86% na 82% mtawaliwa wakiishi vijijini.
Remove ads
Muhtasari
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yenye makao yake makuu Arusha, Tanzania,kazi yake kuu ni kuendeleza muungano wa kiuchumi, kisiasa, na kijamii katika ukanda huu. Mwenyekiti wa sasa wa EAC ni William Ruto, Rais wa Kenya, anayeongoza Mkutano wa Wakuu wa Nchi, ambao ndio chombo cha juu zaidi cha maamuzi katika jumuiya hii.
Kwa miaka iliyopita, EAC imepiga hatua muhimu ikiwemo kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, na mikataba ya kuunda Umoja wa Fedha. Pia imeongeza uanachama wake, ikiwemo kuipokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ,Somalia na Sudan Kusini. Miradi mikubwa ya miundombinu ya kikanda, programu za kurahisisha biashara, na ushirikiano katika sekta za afya na usalama ni miongoni mwa mafanikio yanayoonyesha ushawishi unaokua wa jumuiya hii katika kuendesha mipango ya maendeleo ya Afrika Mashariki.
Remove ads
Historia
Jumuiya ya kwanza
Nchi tatu za Afrika ya Mashariki zilizokuwa chini ya utawala wa Uingereza zilianza uhuru wao kwa kuendeleza ushirikiano wa karibu uliorithiwa kutokana na utawala wa pamoja wakati wa ukoloni.
Baada ya kupata uhuru mwaka 1961 nchi hizo ziliunda Mamlaka ya Huduma za Pamoja za Afrika ya Mashariki (kwa Kiingereza East African Common Services Organisation – kifupi EACSO).
Ushirikiano ulihusu fedha (East African Shilling), forodha (Customs Union), huduma za reli (East African Railway), ndege (East African Airways), mabandari, posta na simu na elimu ya juu (Chuo Kikuu cha Afrika ya Mashariki chenye kampasi Makerere, Dar es Salaam na Nairobi). Mkataba ulilenga pia mahakama kuu ya pamoja na sera ya kiuchumi ya soko la pamoja. Haya yote yalitakiwa kuwa chini ya Bunge la Afrika Mashariki.
Tangu 1965 umoja huo ulianza kurudi nyuma kila nchi ilipoanzisha pesa yake.
Mwaka 1967 nchi tatu zilijaribu upya kuimarisha umoja wao kwa Mkataba wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki wakiita umoja wao "Jumuiya ya Afrika ya Mashariki" ikiwa na makao makuu Arusha, Tanzania.
Lakini mielekeo ya nchi zote tatu zilitofautiana mno: Kenya iliendelea kwa njia ya upebari lakini Tanzania ilijaribu kujenga Ujamaa (usoshalisti) kuanzia mwaka 1967. Uganda uliingia katika kipindi cha udikteta kali ya Idi Amini aliyeharibu uhusiano na majirani alipoanza kudai sehemu za maeneo yao.
Sababu nyingine ni madai ya Kenya ya kuwa na viti zaidi kuliko Uganda na Tanzania katika kamati za maamuzi,[5] huku kukiwa na kutokuelewana kulikosababishwa na udikteta wa Idi Amin nchini Uganda, Usoshalisti huko Tanzania, na soko huria nchini Kenya,[2] hivyo wanachama hawa watatu wakapoteza ushirikiano wa miaka zaidi ya sitini na manufaa ya ukubwa wa jumuiya hii kiuchumi. Kila mmoja wa wanachama hawa ilimbidi kuanza kutoa huduma na kujenga viwanda ambavyo hapo awali vilikuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hivyo mwaka 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikoma kufanya kazi yoyote na 1983 ilifutwa rasmi. Mali iliyobaki iligawanywa kati ya nchi zote tatu.
Kufufuka kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki tangu 1993
Tangu miaka ya 1990 majaribio ya kujenga umoja mpya yalionekana tena.
Marais Daniel arap Moi wa Kenya, Ali Hassan Mwinyi wa Tanzania, na Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda walipatana katika Mkataba wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki huko Arusha, tarehe 30 Novemba 1993, na kuanzisha Tume ya Ushirikiano ya nchi hizi tatu. Shughuli ya kuzileta pamoja nchi hizi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, utafiti na teknolojia, ulinzi, usalama, masuala ya kisheria na kimahakama ilianza.
Mkataba wa kufufua jumuiya ulitiwa sahihi tarehe 30 Novemba 1999 ukaanza kuwa rasmi tarehe 7 Julai 2000.
Vyombo vya Jumuiya mpya ya Afrika ya Mashariki vilianza kufanya kazi mnamo Januari 2001 penye makao makuu ya jumuiya hii huko Arusha.
Mkataba 2004 uliweka msingi wa Umoja wa Forodha ulioanzishwa 2005.
Kuna tena Bunge la Afrika ya Mashariki linalojumuisha wabunge waliochaguliwa na mabunge ya nchi wanachama.
Pia Mahakama Kuu ya Afrika ya Mashariki imeundwa upya.
Mwaka 2008, baada ya majadiliano na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern Africa Development Community, kifupi SADC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Common Market for Eastern and Southern Africa, kifupi COMESA), Mtangamano huo ulikubali nchi zote za miundo hiyo mitatu ziunde eneo pana la biashara huria. Kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mojawapo ya nguzo muhimu za hiyo Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika (African Economic Community, kifupi AEC).
Mwaka 2010, Mtangamano ulitangaza soko la pamoja kwa bidhaa, kazi na mitaji kati ya nchi hizo tano, kwa lengo la kuanzisha pesa ya pamoja na hatimaye Shirikisho kamili.[6]
Kuna majadiliano ya kuanzisha shilingi mpya ya pamoja kwa nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki. Kwanza ilitarajiwa kuanzishwa mwaka 2012, halafu mwaka 2015, sasa mwaka 2024. Mwaka 2013 ulisainiwa mkataba wa kuamua kuanzisha hiyo pesa ndani ya miaka 10.[7]
Remove ads
Uchumi
Pato la taifa
Jumuiya ya Afrika Mashariki ina uchumi unaoendelea ikiwa na Pato la taifa jumla dola bilioni 399 za Marekani kwa Kawaida na trilion 1.197 kwa Usawa wa nguvu ya ununuzi (PPP) hata hivyo ni uchumi wa pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Afrika Kusini. Kenya ndiyo iliyo na uchumi mkubwa zaidi katika jumuiya hii, ikichangia asilimia 37% ya jumla, Tanzania, Kongo, JK zilichangia asilimia 24% na 22% mtawaliwa. Sudan kusini na Burundi ndizo zilizokuwa na uchumi mdogo zaidi. Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ya kipato cha chini ikiwa na pato la taifa kwa kila mtu dola 1,197 . Sudan Kusini ndiyo nchi maskini zaidi ikiwa na pato la taifa kwa kila mtu dola 252 za Marekani, Kenya ndiyo nchi iliyo na pato la taifa kwa kila mtu dola kubwa zaidi ya dola 2,468 za Marekani.
Biashara ya Kimataifa
Mnamo 2023, jumla ya biashara ya kimataifa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilifikia dola bilioni 130.4. Mchango mkubwa zaidi ulitoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (JKK), ambayo ilichangia asilimia 25.8 ya jumla hiyo, ikifuatiwa na Kenya (24.7%) na Tanzania (24.6%). Kwa upande mwingine, nchi zilizo na mchango mdogo zaidi zilikuwa Sudan Kusini (1.8%) na Burundi (0.7%). Kwa Mahuruji (mauzo ya nje) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliongoza zaidi ikichangia asilimia 40% ya mauzo ya nje ya Jumuiya hii, Huku Kenya ikiongoza kwa Maduhuli ikichangia asilimia 30% ya Maduhuli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kati ya nchi zote, Kongo,JK ilikuwa na mizani chanya ya biashara (balance of trade) ya dola bilioni 7.8, ikiwa ya juu zaidi katika kanda, huku Kenya (-16.24), Tanzania (-9.90), na Somalia (-4.22) zikiripoti nakisi kubwa zaidi ya biashara, ishara ya uagizaji mkubwa wa bidhaa kuliko mauzo ya nje.
Remove ads
Nchi Wanachama


Kenya, Tanzania na Uganda zina historia ya ushirikiano tangu mwanzoni mwa karne ya 20, wakati wa ukoloni, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Forodha baina ya Kenya na Uganda mwaka 1917, Tanganyika ilijiunga mnamo mwaka 1927, katika Ubalozi wa Afrika Mashariki (1948-1961), 'East African Common Services Organisation' (1961-1967) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (1967-1977).[10]
Jumuia ambayo ilianzishwa baada ya uhuru ilidumu miaka 10 tu, lakini ilifufuliwa kwa mkataba wa tarehe 30 Novemba 1999, ulioanza kufanya kazi tarehe 7 Julai 2000, miaka 23 baada ya kifo cha ile ya kwanza.
Burundi na Rwanda, ambazo ziliwahi kuwa koloni moja na Tanzania bara kabla ya Vita vikuu vya kwanza, zilijiunga na Mtangamano tarehe 6 Julai 2009.[11]
Mara baada ya kupata uhuru mwaka 2011, Sudan Kusini iliomba kujiunga na Jumuia, lakini haikukubalika hadi Machi 2016 kutokana na hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Tarehe 23 Novemba 2021 Baraza la Mawaziri la EAC limependekeza kwa Wakuu wa nchi wanachama wakubali ombi la kujiunga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo [12], nao wakakubali rasmi tarehe 29 Machi 2022.
Hatua kubwa ya awali katika kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki ni muungano wa forodha katika mataifa husika uliotiwa saini mnamo Machi 2004 na ulioanza kutumika tarehe 1 Januari mwaka 2005. Chini ya masharti ya mkataba, Kenya, ambayo ndiyo nchi inayopata mauzo bora zaidi nje ya nchi katika kanda ya Afrika Mashariki, iliendelea kulipa ushuru kwa bidhaa zake zinazoingia nchi nyingine wanachama hadi mwaka 2010, kwa kiwango kilichopungua na wakati. Mfumo sawa wa ushuru utatumika kwa bidhaa kutoka nchi ambazo si wanachama.
Remove ads
Changamoto
Kwa ujumla, mataifa wanachama kwa kiasi kikubwa wanaona neema ya Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini utafiti usio rasmi unaonyesha kwamba Watanzania wengi (asilimia themanini ya wakazi wake) wana mtazamo hasi.[13]
Tanzania imekuwa na historia ya amani tangu kunyakua uhuru, ikilinganishwa na fujo na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoshuhudiwa katika mataifa ya Kenya, Rwanda, Burundi, na Uganda. Wakati huu Afrika Mashariki inajaribu kudumisha utulivu na mafanikio katikati ya migogoro inayoendelea katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Pembe ya Afrika na Sudan Kusini.
Pia ni kwamba Tanzania ina ardhi kubwa, na baadhi ya Watanzania wana hofu ya unyakuzi wa ardhi na wakazi wa sasa wa mataifa mengine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.[14] [15] [16]
Uhaba wa ardhi ni suala nyeti katika eneo la Afrika Mashariki, hasa nchini Kenya, ambako mapigano ya wenyewe kwa wenyewe upande wa Mlima Elgon mwaka 2007 yaliwaacha zaidi ya watu 150 wamefariki na kulazimisha takriban watu wengine 60,000 kugura makazi yao.[17]
Remove ads
Serikali na Utawala
Mahakama ya Afrika Mashariki
Mahakama ya Afrika Mashariki ndiyo mahakama inayosimamia kesi zote katika eneo hilo. Kwa sasa imo mjini Arusha, Tanzania.
Bunge la Afrika Mashariki
Bunge la Afrika Mashariki ndicho kitengo cha kutengeneza sheria katika eneo la Afrika Mashariki. Ina wajumbe 27 ambao wote wamechaguliwa na mabunge ya nchi wanachama. Linahusika na masuala yote ambayo yanahusu Jumuiya hii kama vile kujadili bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yote ya Jumuiya na kutoa mapendekezo kwa Baraza juu ya mambo wanayoyadhani muhimu kwa utekelezaji wa mkataba, kushirikiana pamoja na Bunge husika na kuanzisha kamati kwa makusudi kama vile wanavyodhani ni muhimu. Tangu uzinduzi wake mwaka 2001, bodi hii imekuwa na vikao kadhaa mjini Arusha, Kampala na Nairobi.
Remove ads
Viungo
Pasipoti ya Afrika Mashariki
Pasipoti ya Afrika Mashariki ilizinduliwa rasmi tarehe 1 Aprili 1999 ili kurahisisha usafiri na kuvuka mipaka ya nchi husika.[18][19] Ni halali kwa kusafiri ndani ya eneo la Afrika Mashariki (Kenya,Uganda na Tanzania) na kutoa haki ya kuingia na kukaa kwa miezi sita katika nchi yoyote na kisha unaweza ukaitumia tena.[18] Pasipoti hii inapatikana katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji katika miji ya Nairobi, Kampala na Dar es Salaam. Ni raia tu wa Afrika Mashariki wanaoweza kuomba pasipoti hii.[18][19] Gharama ya pasipoti hii ni dola 10 za Marekani au pesa sawa ukibadilisha kwa sarafu za nchi za Afrika mashariki.[19] Baada ya kujaza fomu za kupata pasipoti hii itachukua muda wa wiki mbili au tatu kuipata tayari kwa matumizi. Ingawa pasipoti hii ni halali tu ndani ya Afrika Mashariki, majadiliano yalifanywa ili kuwa na hati sawa za kusafiri kwa watu wote wa Afrika Mashariki.[18]
Viza moja kwa watalii
Lilikuwa tarajio la wengi kuwa kabla ya 2006 kungekuwa na viza moja kwa watalii wote wanaozuru Afrika Mashariki, iwapo mpango huo ungeidhinishwa na mamlaka ya sekta husika chini ya jumuiya hiyo. Iwapo ingekubalika basi viza hiy ingetumika kote katika ardhi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Chini ya pendekezo hili viza yoyote mpya ya Afrika Mashariki ingeweza kupokewa kutoka ubalozi wowote katika eneo la Afrika Mashariki.
Mtandao
Matumizi ya wavuti katika eneo la Afrika Mashariki bado yako chini mno yakilinganishwa na mataifa yaliyostawi kiuchumi.
Eneo la Afrika Mashariki ni kituo kizuri kiuchumi huku likikadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni 150. Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya wakazi wa Afrika Mashariki - milioni 15 - huutumia Mtandao.
Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unasisitiza ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo kwa kuzingatia uwezo wa kijamii.
Wengi wa wakazi wa Afrika Mashariki hutumia mtandao kuangalia habari, kusoma barua pepe na kwenye mitandao mingine ya kijamii.
Hivi karibuni kumekuwa na majukwaa mengi yanayoibuka katika eneo hili kwa lengo la kuileta pamoja Afrika Mashariki.
Kasi ya mawasiliano kupitia kwa mtandao pia iko chini mno katika eneo la Afrika Mashariki, ikilinganishwa na mataifa yaliyostawi. Hii labda ni mojawapo ya vikwazo vya maendeleo ya mawasiliano ya mtandao Afrika Mashariki.
Remove ads
Jiografia
Mtangamano ungekuwa nchi moja tu, ungekuwa ya 7 duniani kwa eneo (kilometa mraba 4,812,618).
Ziwa Victoria kati ya nchi za Mtangamano.
Mlima Kilimanjaro, mrefu kuliko yote ya Afrika, uko Tanzania.
Sudan Kusini, Uganda, Rwanda na Burundi hazina pwani baharini, lakini zina mvua za kutosha.
Huku inapatikana minne kati ya milima mirefu zaidi barani Afrika: Mlima Kilimanjaro (Tanzania), Mlima Kenya (Kenya), milima ya Rwenzori (Uganda/DRC) na Mlima Meru (Tanzania).
Ziwa Turkana, Kenya, ndiyo ziwa la jangwani kubwa na lenye maji ya chumvi nyingi kuliko yote duniani.
Ziwa Victoria linaunganisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania na ni la pili duniani kwa eneo.
Ziwa Tanganyika kati ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni la pili duniani kwa kina.
Kenya pekee ina jangwa, jangwa la Chalbi katika Kaunti ya Marsabit.
Dar es Salaam, ukiwa na watu milioni 4 ndio mji mkubwa kuliko yote ya Mtangamano baada tu ya Kinshasa.
Ugatuzi katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (E.A.C.)
Burundi
Kenya
- Mombasa
- Kwale
- Kilifi
- Tana River
- Lamu
- Taita–Taveta
- Garissa
- Wajir
- Mandera
- Marsabit
- Isiolo
- Meru
- Tharaka-Nithi
- Embu
- Kitui
- Machakos
- Makueni
- Nyandarua
- Nyeri
- Kirinyaga
- Murang'a
- Kiambu
- Turkana
- West Pokot
- Samburu
- Trans-Nzoia
- Uasin Gishu
- Elgeyo-Marakwet
- Nandi
- Baringo
- Laikipia
- Nakuru
- Narok
- Kajiado
- Kericho
- Bomet
- Kakamega
- Vihiga
- Bungoma
- Busia
- Siaya
- Kisumu
- Homa Bay
- Migori
- Kisii
- Nyamira
- Nairobi
Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia
- Mkoa wa Équateur
- Mkoa wa Ituri
- Mkoa wa Kasai
- Mkoa wa Kasai Kati
- Mkoa wa Kasai Mashariki
- Mkoa wa Katanga Juu
- Mkoa wa Kinshasa
- Mkoa wa Kivu Kaskazini
- Mkoa wa Kivu Kusini
- Mkoa wa Kongo Kati
- Mkoa wa Kwango
- Mkoa wa Kwilu
- Mkoa wa Lomami
- Mkoa wa Lomami Juu
- Mkoa wa Lualaba
- Mkoa wa Mai-Ndombe
- Mkoa wa Maniema
- Mkoa wa Mongala
- Mkoa wa Sankuru
- Mkoa wa Tanganyika
- Mkoa wa Tshopo
- Mkoa wa Tshuapa
- Mkoa wa Ubangi Kaskazini
- Mkoa wa Ubangi Kusini
- Mkoa wa Uele Chini
- Mkoa wa Uele Juu
Rwanda
Somalia
Sudan Kusini
Tanzania
Uganda
Remove ads
Tazama pia
- Orodha ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Pato la taifa
- Orodha ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Kiashiria cha Maendeleo ya Binadamu
- Orodha ya Maeneo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Kiashiria cha Maendeleo ya Binadamu
- Orodha ya nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki kulingana na Umri wa Kuishi
- Shirikisho la Afrika Mashariki
- Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
- Uchumi wa Afrika
- Mamlaka ya Maendeleo ya Kitaifa (IGAD)
- Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
- Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA)
- Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Kati (ECCAS)
- Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Tanzania
Remove ads
Tanbihi
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Remove ads